DAR ES SALAAM
Wakati maandalizi ya Mkutano wa Nishati wa Wakuu wa Nchi za Afrika (Mission 300) yakiwa kwenye hatua za mwisho, Jiji la Dar es Salaam limeonyesha dhamira ya kuandika historia kwa kufanikisha tukio hili muhimu la kimataifa. Mkutano huo, unaotarajiwa kufanyika Januari 27-28, 2025, utawakutanisha viongozi wa nchi 54 za Afrika, wataalamu, na wadau wa sekta ya nishati, ukilenga kujadili njia za kuimarisha ushirikiano wa bara hili katika sekta ya nishati.
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, ameweka msisitizo mkubwa katika kuhakikisha mji mkuu wa kibiashara wa Tanzania unakuwa mwenyeji bora kwa wageni. Akizungumza jana, Januari 11, 2025, wakati wa kampeni ya usafi katika Soko la Samaki la Feri, RC Chalamila alisema maandalizi yanapiga hatua kubwa, huku usalama na usafi vikiwa kipaumbele.
RC Chalamila ameonya vikali dhidi ya vitendo vya kihalifu wakati wa maandalizi na kipindi cha mkutano. “Natoa onyo kwa vibaka wote! Katika kipindi hiki, hatua kali zitachukuliwa kwa yeyote atakayekiuka sheria. Hii ni fursa ya Tanzania kujitangaza kimataifa, hatutakubali yeyote kuharibu sifa ya nchi yetu,” alisema kwa msisitizo.
Aidha, alihimiza wananchi kuutumia mkutano huu kama fursa ya kukuza biashara zao kwa kuhakikisha mazingira yao ya kazi yanavutia. “Usafi si jambo la hiari tena. Huu ni wakati wa kuonyesha uzalendo na kuunga mkono juhudi za serikali,” aliongeza.
Ili kuhakikisha mkutano huo unafanikiwa, serikali imeboresha miundombinu katika maeneo ya mkutano, ikiwemo kuboresha taa za barabarani na kuzifunga barabara kadhaa kwa usafiri wa bajaji na bodaboda ili kuwezesha wageni na viongozi kufanikisha ratiba zao kwa urahisi.
“Rais Samia Suluhu Hassan ameifungua Tanzania kwa ulimwengu, na mkutano huu ni moja ya matokeo ya juhudi zake za kuifanya nchi yetu kuwa kitovu cha maendeleo ya kimataifa,” alisema RC Chalamila.
Mkutano wa Mission 300 sio tu fursa ya kujadili mustakabali wa nishati barani Afrika, bali pia nafasi ya Dar es Salaam kujitangaza kama kituo cha mikutano ya kimataifa, kukuza uchumi, na kuimarisha ushirikiano wa kidiplomasia na nchi zingine za Afrika.