OR-TAMISEMI, Tunduma
Kamati ya kudumu ya Bunge ya TAMISEMI imeipongeza Halmashauri ya Mji Tunduma kwa kutumia mapato ya Ndani kujenga shule ya Sekondari ya Uwanjani.
Pongezi hizo zimetolewa na Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe.Justin Lazaro Nyamoga mara baada ya kukagua mradi wa ujenzi wa shule hiyo mpya sekondari Uwanjani iliyojengwa katika muundo wa gorofa kupitia mradi wa sequip na fedha zitokanazo na mapato ya ndani zaidi ya shilingi Bil. 1.
Amezitaka Halmashauri ambazo zinakusanya mapato ya ndani mapato makubwa kuiga mfano huo kwa kutekeleza miradi yao na sio kusubiri fedha kutoka Serikali kuu pekee ili kuendelea kurahisisha upatikanaji wa huduma kwa wananchi.
Aidha, Mhe. Nyamoga amezishauri Halmashauri zenye idadi kubwa ya watu kuanza kujenga miradi ya majengo ya Serikali na taasisi za Serikali kwa muundo wa gorofa ili kuendelea kutunza ardhi kwa matumizi ya vizazi vijavyo.
Akizungumza kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais – TAMISEMI Mhe. Mohamed Mchengerwa, Naibu Waziri Ofisi ya Rais – TAMISEMI Mhe. Zainab Katimba amepokea ushauri huo wa Kamati huku akuahidi kufanyia kazi ushauri huo ili miradi hiyo iendelee kuwanufaisha wananchi kiuchumi na kijamii.