………………
Na Sixmund Begashe – Mlele
Maafisa na Askari wa Jeshi la Uhifadhi nchini wametakiwa kujiepusha na vitendo viovu vya aina yoyote ikiwemo rushwa wakati wa kutekeleza majukumu yao ya Uhifadhi ili kuepuka madhara makubwa yanayoweza kuwapata wao wenyewe, familia zao na Taifa kwa ujumla.
Wito huo umetolewa na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii anaeshughulikia Maliasili, Kamishna wa Polisi, Benedict Wakulyamba, alipokuwa akiongea na Wakufunzi na wanafunzi wa kozi namba 3 ya mafunzo ya Mabadiliko ya utendaji (Transformation course) katika Kituo cha Mafunzo ya Jeshi la Uhifadhi Mlele, Mkoani Katavi.
CP. Wakulyamba amesema kuwa shughuli za uhifadhi wa Maliasili nchini zinatakiwa zitekelezwe kwa nidhamu ya hali ya juu kwa kuwa vitendo vya rushwa havikubaliki kwa maslai mapana ya Taifa kwa ujumla.
Amesisitiza kuwa, uongozi wa Wizara hiyo hautakuwa na muhali kwa yeyote katika Jeshi hilo atakaejihusisha na vitendo vya rushwa kwa kuwa vinakinzana na maadili ya utumishi wa Kijeshi na pia zinadhoofisha jitihada za Serikali katika uhifadhi endelevu wa Maliasili za watanzania.
“Serikali yetu chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye ni Mhifadhi namba moja nchini, inafanya kazi kubwa ya Uhifadhi wa Maliasili hizi tulizonazo, ambazo tumepewa kazi tuzisimamie, hivyo hatuwezi kukubali kuona mtumishi anahujumu Maliasili hizi kwa njia yeyote na kwa maslahi yake binafsi hususan rushwa, tukamuacha, tutamshughulikia” Alisisitiza CP. Wakulyamba
Aidha CP. Wakulyamba amesema kuwa tabia ya rushwa ni ya ubinafsi na madhara yake ni makubwa kwani hupelekea maumivu kwa kizazi cha sasa na kijacho. Pindi mtumishi anapofukuzwa kazi kwa sababu za rushwa athari zake huikumba familia hususani watoto, Mke au mme hivyo ni vyema watumishi kuepukana na rushwa ili kuzuia madhara hayo kwao na familia zao
Akiongea na wanafunzi wa kozi ya awali namba 11 ya ajira mpya TANAPA, CP. Wakulyamba amewapongeza kwa kupata nafasi ya kujiunga na mafunzo hayo adhimu huku akiwataka kuzingatia mafunzo wanayopata ili wawe wahifadhi bora, watendaji wenye nidhamu, weledi na uadilifu mkubwa wanaozingatia Utawala bora na haki za binadamu watakapoajiriwa kwa maslai mapana ya Maliasili na nchi kwa ujumla.
Katika ziara hiyo yenye lengo la kuliboresha na kuliimarisha Jeshi la Uhifadhi, wakufunzi wabobezi kutoka Jeshi la Polisi walitoa mafunzo mbalimbali yakiwemo Umiliki na matumizi sahihi ya Silaha, haki za binadamu na utawala wa sheria pamoja na Misingi ya nguzo muhimu za Jeshi ikiwemo nidhamu na uadilifu mahala pa kazi.