Dar es Salaam.
Askofu Dkt. Alex Malasusa, Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), ameimwagia sifa Ofisi ya Msajili wa Hazina kwa mageuzi makubwa na ya haraka yanayoendelea katika usimamizi na uendeshaji wa mashirika ya umma chini ya uongozi wa Bw. Nehemiah Mchechu, Msajili wa Hazina.
Askofu Malasusa ametoa pongezi hizo leo, Januari 11, 2025, katika Ibada maalumu iliyoandaliwa na familia ya Bw. Mchechu mahususi kwaajili ya kumshukuru Mungu kwa ulinzi na baraka za mwaka 2024 na kuomba rehema na neema zaidi katika mwaka mpya wa 2025.
Ibada hiyo iliyofanyika katika Kanisa la KKKT, Usharika wa Mbezi Beach, imefanikisha kukusanya zaidi ya Sh70 milioni ikiwa ni sadaka maalumu ya ujenzi wa Kanisa.
Katika ibada hiyo iliyoendeshwa na Mchungaji Allen Mbiso na kushirikisha familia, ndugu, jamaa na marafiki, ikiwemo baadhi ya watumishi wa Ofisi ya Msajili wa Hazina, Askofu Malasusa alisema siku zote Bw. Mchechu amekuwa mtu wa kuleta mabadiliko popote anapofanya kazi.
“Hata sisi hapa kwetu kwa kipindi chote alichotumika kama Mwenyekiti wa Kamati ya Fedha na Mipango, Dayosisi ya Mashariki na Pwani, kisha Katibu wa Usharika wa Mbezi Beach, daima amekuwa mtu wa mabadiliko,” alisisitiza Askofu Malasusa.
Kwa upande wake Bw. Mchechu akielezea sababu ya kuomba misa hiyo maalumu ya shukrani alisema imekuwa ni utaratibu wa familia yake kurudi katika madhabahu kushukuru kwa yote ambayo Mungu amekuwa akitenda katika maisha yao.
Bw. Mchechu alitolea mfano wa hadithi katika biblia takatifu, kitabu cha Luka 17:11 inayowahusu watu 10 wenye uhitaji waliobarikiwa na Yesu Kristo lakini ni mmoja tu kati yao ndiye alierudi kushukuru kwa kile alichotendewa na kusema kila mtu ana sababu ya kusema asante katika kila jambo.
Hadithi hiyo inaeleza kuwa Yesu akiwa safarini kwenda Yerusalemu alipitia katika mipaka ya Samaria na Galilaya.
Alipokuwa anaingia katika kijiji kimoja, watu kumi wenye ukoma walikutana naye, wakasimama kwa mbali—wakapaza sauti wakisema, “Yesu Mwalimu, tuonee huruma”.
Alipowaona akawaambia, nendeni mkajioneshe kwa makuhani. Basi, ikawa walipokuwa wanakwenda, wakatakasika.
Mmoja wao alipoona kwamba ameponywa, alirudi akimtukuza Mungu kwa sauti kubwa. Akajitupa chini mbele ya miguu ya Yesu huku akimshukuru.
Huyo alikuwa Msamaria. Hapo Yesu akasema, “Je, si watu kumi walitakaswa? Wale tisa wako wapi? Hakupatikana mwingine aliyerudi kumtukuza Mungu ila tu huyu mgeni?”
Kutokana na kitendo alichofanya mgeni huyo, Yesu alimwambia, “simama, uende zako; imani yako imekuponya.