DAR ES SALAAM
NA JOHN BUKUKU
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, ametangaza kampeni kubwa ya usafi na uboreshaji wa mazingira katika maeneo yote muhimu ya jiji kuelekea Mkutano wa Wakuu wa Nchi za Afrika kuhusu Nishati, maarufu kama Africa Energy Summit. Mkutano huo unatarajiwa kufanyika tarehe 27 na 28 Januari 2025 katika Ukumbi wa Julius Nyerere (JNICC).
Akizungumza na waandishi wa habari, Chalamila alieleza kuwa kampeni hiyo inalenga kuboresha mwonekano wa jiji, hususan katika maeneo muhimu kama Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, fukwe za Bahari ya Hindi, Posta, Mwenge, na barabara kuu ambazo zitapitwa na viongozi wa Afrika wanaotarajiwa kushiriki.
“Tunataka taswira ya Tanzania iwe ya kuvutia na kuonyesha maendeleo tuliyofikia,” alisema Chalamila.
Katika hatua ya kuhakikisha jiji linapendeza, majengo yaliyopo kando ya barabara hizo yameanza kufanyiwa ukarabati. Tayari zaidi ya nyumba 10 kati ya 30 zinazosimamiwa na Shirika la Nyumba la Taifa zimesafishwa na kukarabatiwa.
Aidha, Chalamila alitangaza kuwa maroli yote hayatakuwa na ruhusa ya kupaki kando ya barabara baada ya tarehe 20 Januari 2025 ili kuhakikisha usalama na mwonekano mzuri wa jiji.
Mkutano wa Africa Energy Summit unalenga kujadili masuala ya nishati safi barani Afrika. Moja ya malengo yake ni kuhakikisha watu milioni 300 wanaunganishwa na huduma za umeme ifikapo mwaka 2030, hatua inayochagiza dhamira ya Rais wa Tanzania ya kuhakikisha matumizi ya nishati safi kwa kila kaya. Hatua hii inaiweka Tanzania katika nafasi ya uongozi kwenye mapinduzi ya nishati barani Afrika.