Na Fauzia Mussa
Waziri wa Afya Zanzibar, Nassor Ahmed Mazrui, amesema kuwa maendeleo yanayoendelea katika sekta ya utalii nchini ni utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na maono ya Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Dk. Hussein Ali Mwinyi.
Mazrui alitoa kauli hiyo wakati akifungua rasmi mradi wa villa za Heritage Sunset Retreat huko Fukuchani, Wilaya ya Kaskazini A, Mkoa wa Kaskazini Unguja. Hafla hiyo ilikuwa sehemu ya shamra shamra za maadhimisho ya miaka 61 ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mazrui alisema mradi huo unalenga kuongeza pato la mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla, sambamba na kuonyesha matunda ya Mapinduzi ya mwaka 1964. Aliwataka vijana wa Shehia ya Fukuchani kusomea fani za utalii na historia ili waweze kunufaika na ajira zinazotokana na mradi huo.
“Mradi huu wa kihistoria utatoa fursa za ajira kwa jamii ya Fukuchani na maeneo jirani pamoja na kukuza uchumi wa Taifa kupitia harakati za kitalii. Sio vyema kuona wafanyakazi wa eneo hili wanatoka mbali, hivyo vijana niwasihi msomee fani za utalii na historia ili kunufaika na mradi huu uliopo katika kijiji chenu,” alisema Mazrui.
Aidha, Waziri huyo alishauri Wizara husika kufanya utafiti wa kina ili kubaini na kukarabati maeneo mengine ya kihistoria kwa ajili ya kuongeza idadi ya vivutio vya utalii nchini na kupanua fursa za ajira kwa jamii.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Utalii na Mambo ya Kale, Dk. Amina Ameir Issa, alisema eneo la Fukuchani ni mojawapo ya maeneo 86 ya kihistoria yaliyotangazwa katika Gazeti Rasmi la Serikali. Alifafanua kuwa maeneo hayo yanajumuisha majengo ya kale ya ngome ya Wareno na makaburi ya kihistoria, yakiwemo makaburi ya mtu maarufu aliyeitwa “Banja Faraja.”
Kwa mujibu wa Dk. Amina, eneo hilo lilikuwa bandari maarufu wakati wa utawala wa Wareno mnamo miaka ya 1600. Wareno walijenga mnara wa kuangalia maadui kwa ajili ya usalama wa makazi ya watu na walijihusisha na kilimo cha tumbaku na mazao mengine ya chakula.
Alieleza kuwa mwaka 1941, Serikali ya Kikoloni ya Waingereza iliorodhesha maeneo hayo kama sehemu za kihistoria kwa mujibu wa Sheria ya Uhifadhi wa Majengo ya Kale ya mwaka 1927. Baada ya Mapinduzi ya mwaka 1964, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ilianza kuhifadhi maeneo hayo kwa ajili ya urithi wa kihistoria.
Dk. Amina alieleza kuwa ujenzi wa mradi wa Heritage Sunset Retreat ulianza mwaka 2023 na unatarajiwa kukamilika mwaka 2025, ambapo umefikia asilimia 40 ya utekelezaji. Mradi huu unagharimu Dola milioni 2 za Kimarekani hadi kukamilika kwake.
Mradi huo unahusisha awamu tatu za ujenzi wa villa nane:
1. Awamu ya Kwanza: Ujenzi wa villa tatu za vyumba sita zenye bwawa la kuogelea, bustani, na sehemu za kuegesha magari. Awamu hii tayari imekamilika kwa gharama ya Dola 800,000.
2. Awamu ya Pili: Ujenzi wa villa mbili za vyumba sita pamoja na eneo la kupokelea wageni kwa gharama ya Dola 500,000.
3. Awamu ya Tatu: Ujenzi wa villa tatu za vyumba 10 kwa gharama ya Dola 700,000.
Dk. Amina aliongeza kuwa wananchi wa Fukuchani na vijiji jirani wamelipwa fidia za mali zao zilizokuwepo eneo la mradi, huku wakipata fursa za ajira kwenye ujenzi na usambazaji wa bidhaa kama samaki, mboga, na matunda.
Mwekezaji wa mradi huo, balozi wa heshima wa Ufaransa, Yves Montalles, aliishukuru Serikali na wananchi wa Fukuchani kwa ushirikiano wao uliomrahisishia uwekezaji. Yves aliahidi kutoa nafasi za masomo ya utalii kwa vijana wa Fukuchani ili wanufaike zaidi na mradi huo.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Kaskazini A, Rashid Simai Msaraka, alisema usalama na amani vimechochea maendeleo ya utalii katika Mkoa huo. Aliwasihi wananchi kuendelea kudumisha utulivu huo ili kufanikisha maendeleo zaidi.
Msaraka aliongeza kuwa juhudi za Rais Dk. Hussein Mwinyi zimeleta Mapinduzi makubwa katika sekta ya utalii, ambayo yameongeza fursa za maendeleo kwa wananchi wa Zanzibar.