DAR ES SALAAM
Serikali kupitia Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, imewataka wafanyabiashara wa mkoa huo kufanya biashara zao kwa saa 24 wakati wa Mkutano wa Wakuu wa Nchi za Afrika kuhusu Nishati, unaotarajiwa kufanyika Januari 27-28, 2025. Ugeni huo wa zaidi ya mataifa 30 utahitaji huduma mbalimbali za kijamii kama vile chakula na malazi.
Akizungumza leo Januari 9, 2025, wakati akikagua miundombinu ya barabara ya Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), Chalamila amesema tarehe maalum na rasmi ya kuanza biashara masaa 24 itatangazwa hivi karibuni.
Aidha, ametoa agizo kwa wamiliki wa malori kuhakikisha kuwa magari hayo hayapo pembezoni mwa barabara ifikapo Januari 20, 2025. “Malori ni muhimu sana kwa uchumi wetu, yanatoa ajira na kukuza mapato ya nchi, lakini yakiachwa bila mpangilio, yanaharibu taswira ya mji. Tumekubaliana kabisa kuwa pembezoni mwa barabara hakutakuwa na malori,” alisema Chalamila.
Pia, Chalamila amesema serikali imewekeza kikamilifu katika sekta ya afya, na wakati wa mkutano huo, madaktari na hospitali kubwa jijini Dar es Salaam wataonyesha maendeleo makubwa yaliyofanyika. Aliwataja viongozi wa hospitali mbalimbali, akiwemo Dkt. Peter Kisenge wa JKCI, Prof. Mohamed Janabi wa Muhimbili, na viongozi wa Moi na Ocean Road, kuwa watashiriki kuonyesha mafanikio ya uwekezaji katika sekta hiyo.
Mkutano huo wa Wakuu wa Nchi za Afrika kuhusu Nishati utafanyika katika Ukumbi wa Julius Nyerere (JNICC), jijini Dar es Salaam, na unatarajiwa kuwa fursa kubwa kwa mkoa huo kuonyesha uwezo wake katika kutoa huduma bora kwa wageni.