Na Mwandishi Wetu
MWENYEKITI wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba amewaelekeza wajumbe wa Baraza Kuu la chama hicho kushiriki kikamilifu katika mchakato wa kuandaa Ilani ya Uchaguzi wa 2025 ya chama, pamoja na kudai Katiba Mpya.
Aidha Prof Lipumba amewataka wajumbe hao kwenda kusimamia rasilimali za nchi ili ziweze kuwa na manufaa na wananchi wote.
Lipumba ametoa maelekezo hayo leo wakati akifungua Kikao cha Nane cha Baraza Kuu la chama hicho kilichofanyika katika Ukumbi wa Shaban Mloo, Buguruni wilayani Ilala mkoani Dar es Salaam
“Wajumbe wa Baraza Kuu ndio viongozi wa kusimamia sera ya CUF ya haki sawa na furaha kwa wote, hivyo nawaomba wakati tukiunda kamati ya kuandaa Ilani muipe ushirikiano wa hali na mali ikiwa kuhakikisha ilani yetu inakuwa bora,” amdsema.
Lipumba amesema CUF ndio chama kinaweza kuleta mabadiliko chanya kwa nchi na jamii, hivyo ni vema ilani yao ikidhi vigezo muhimu katika kuleta mabadiliko.
Amesema katika uandaaji wa ilani hiyo watatumia ilani iliyopita kuangalia yale ambayo yanapaswa kuingizwa nkwa kuongoza nguvu kazi ya kusimamia rasilimali .
Aidha aliwataka wajumbe hao wa Baraza Kuu kuhakikisha wanatoa elimu na kuhamasisha wananchi umuhimu wa kupata Katiba Mpya ambayo itagusa mahitaji ya wananchi.
“Napenda kutumia nafasi hii ya kikao cha Baraza Kuu la chama kuomba kila mmoja ashiriki kikamilifu katika kuhakikisha Ilani ya CUF 2025 inakuwa yenye ubora, lakini kubwa zaidi nawaomba tupiganie Katiba mpya kwani ndio inaweza kuondoa changamoto zote ambazo zipo nchjni ikiwemo uchaguzi,” amesema.
Mwenyekiti huyo amesema chama chai kinatarajia kuja na ilani ambayo itaunganisha wananchi na viongozi wake ili kuchochea maendeleo.
Lipumba amesema uchaguzi wa serikali za mitaa umeonesha namna ambavyo Katiba ya sasa inachangia kuzuia haki za wananchi kuchagua, hivyo ni wakati muafaka kwa kila mpenda haki sawa na furaha kwa wote kushiriki kudai Katiba Mpya.
Mwenyekiti huyo ameweka wazi iwapo wananchi watawapa ridhaa ya kuingoza Tanzania 2025 watahakikisha kunakuwa na Serikali ya Umoja wa Kitaifa kwa vyama vyote kushiriki kuunda serikali.
Kwa upande mwingine Lipumba amesema hali ya demokrasia mbini na dunia kwa ujumla imeporomoka, hivyo vyama vya siasa na asasi za kidemokrasia kuweka nguvu.
“Hali ya demokrasia duniani inaporomoka toka 2006.
Hata Marekani demokrasia imeporomoka na mfano hai uchaguzi wa 2020 Rais Donald Trump
Amesema Tanzania demokrasia imeporomoka na uchaguzi wa serikali za mitaa umethibitisha hilo.
Taarifa ya uchaguzi iliyotolewa na waziri wa TAMISEMI iliandalia siku moja kabla ya siku ya uchaguzi.
Amesema Rais Samia Suluhu Hassan ambaye alikuja na 4R ameshindwa kuzisimamia na ushahidi ni uchaguzi wa serikali za mitaa ambao umekiuka kanuni na sheria za uchaguzi.
Lipumba amesema uvumilivu wa watanzania una kikomo, hivyo kuwataka watawala kuzingatia haki sawa kwa wote ila kuepusha migongano baina yao.
“Misingi ya CUF ni haki sawa kwa wote na furaha, iwapo watawala watapuuza uvumilivu wa Watanzania itakoma na tutaongea mengine wakati huo, sisi hatutaki kufika huko,” amesema.
Amesema hali ya maisha kwa sasa ni ngumu jambo ambalo linapelekea vijana wengi kuonekana wazee, hivyo kuishauri serikali kuwekeza kwa vijana.
Lipumba amesema sekta ya elimu nayo imekuwa haina faida kwa vijana kwani bado ipo katika misingi ya kizamani jambo ambalo linatakiwa kuangaliwa upya.
Kwa upande mwingine Lipumba ameitaka serikali iboreshe sekta afya hasa katika eneo la mama wajawazito na watoto kwani takwimu zinaonesha bado vifo ni vingi.
Amesema iwapo serikali itatumia rasilimali misitu, wanyama, ardhi, madini na nyingine Tanzania itapata maendeleo ya haraka.
Aidha ameitaka serikali kuwekeza kwenye viwanda ili kuweza kulisha nchi jirani na kuongeza ajira.