Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Bw. Emmanuel Tutuba akitangaza uamuzi wa Kamati ya Sera ya Fedha ya Benki Kuu ya Tanzania kuhusu kuendelea na kiwango cha Riba ya Benki Kuu (CBR) cha asilimia 6 kwa robo ya kwanza ya mwaka 2025.
Naibu Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (Sera za Uchumi na Fedha), Dkt. Yamungu Kayandabila, akishiriki katika mkutano huo.
Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Bw. Emmanuel Tutuba katikati akiwa pamoja na Naibu Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (Sera za Uchumi na Fedha) Dkt. Yamungu Kayandabila wa pili kutoka kushoto na wa pili kutoka kulia ni Naibu Gavana, Utawala na Udhibiti wa Ndani, Bw. Julian Banzi Raphael pamoja na mkurugenzi wa Utafiti BoT Dkt. Suleiman Misango
………………
Kamati ya Sera ya Fedha ya Benki Kuu ya Tanzania imeamua kuendelea na kiwango cha Riba ya Benki Kuu (CBR) cha asilimia 6 kwa robo ya kwanza ya mwaka 2025.
“Uamuzi huo wa Kamati wa kutokubadili Riba ya Benki Kuu unalenga kuhakikisha kiwango cha ukwasi kinaendelea kuwa cha kutosha katika uchumi, kudhibiti mfumuko wa bei kubaki chini ya lengo la asilimia 5, na kuwezesha kuongezeka kwa kasi ya ukuaji wa uchumi kufikia takriban asilimia 5.7 katika robo ya kwanza ya mwaka 2025,”
Hayo yameelezwa leo Januari 08, 2025 na Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Bw. Emmanuel Tutuba wakati akitangaza uamuzi huo mbele ya wakuu wa benki na taasisi za fedha pamoja na waandishi wa habari tarehe 8 Januari 2025 jijini Dar es Salaam kufuatia kikao cha Kamati ya Sera ya Fedha kilichofanyika tarehe 7 Januari.
Aidha, amesema uamuzi huo ambao umefikiwa kutokana na tathmini iliyofanywa ya mwenendo wa hali ya uchumi wa dunia na hapa nchini, unalenga kuwa na utulivu wa thamani ya shilingi dhidi ya fedha za kigeni ili kuendelea kuwa na mfumuko wa bei mdogo.
“Utulivu wa thamani ya shilingi dhidi ya fedha za kigeni utachangia katika juhudi za kufanya wananchi kutofanya miamala kwa kutumia fedha za kigeni nchini,” amese Gavana Tutuba.
Kuhusu mwenendo wa uchumi wa dunia, Kamati ya Sera ya Fedha imesema ripoti za Shirika la Fedha Duniani (IMF) na Benki ya Dunia, zinaonesha ukuaji wa uchumi unakadiriwa kuwa imara katika mwaka 2024.
Aidha, mazingira ya uchumi duniani katika robo ya nne ya mwaka 2024 yaliimarika kwa kiwango kikubwa, ambapo kasi ya ukuaji wa uchumi iliongezeka, mfumuko wa bei uliendelea kupungua katika nchi nyingi, na mazingira ya upatikanaji wa fedha kwa riba nafuu katika masoko yaliimarika.
“Bei za bidhaa katika soko la dunia, hususan mafuta ghafi, zilipungua. Hali hii ilichangia kuimarika kwa uchumi wa Tanzania. Mazingira haya mazuri ya kiuchumi yanatarajiwa kuendelea katika robo ya kwanza ya mwaka 2025 kutokana na ongezeko la mahitaji ya walaji, sera wezeshi za bajeti na kuimarika kwa mazingira ya upatikanaji fedha kwa riba nafuu,” ameeleza Gavana Tutuba.
Hata hivyo, matarajio hayo mazuri ya uchumi yanaweza kuathirika endapo migogoro ya kisiasa duniani na mivutano ya kibiashara itaongezeka.
Katika kikao hicho, Gavana Tutuba amesema, Kamati imeridhishwa na mwenendo wa uchumi wa hapa nchini kutokana na utekelezaji madhubuti wa sera za fedha na bajeti na maboresho ya kukuza uchumi.
“Kuimarika kwa mazingira ya kiuchumi duniani yamechangia kuendelea kuimarika kwa uchumi. Kuimarika kwa uchumi pia kulithibitishwa katika tathmini iliyofanywa na Kampuni ya Fitch Ratings mwezi Disemba 2024, ambapo uchumi umendelea kubakia katika alama ya B+ yenye matarajio ya kuendelea kuimarika,” amesema Bw. Tutuba.
Vilevile, IMF imeonesha kuridhika na mwenendo wa uchumi katika tathmini ya programu za Extended Credit Facility (ECF) na Resilience and Sustainability Trust (RST).
“Benki Kuu itaendelea kuhakikisha uwepo wa ukwasi unaoendana na mahitaji ya uchumi, ili kufikia malengo ya kuwa na mfumuko wa bei mdogo na kuchagiza ukuaji wa shughuli za uchumi. Katika kufikia malengo haya, Benki Kuu itaendelea kufuatilia mwenendo wa uchumi na kuchukua hatua stahiki pale itakapohitajika,” amesema Gavana ambaye pia ni mwenyekiti wa Kamati ya Sera ya Fedha.