Mbunge wa Jimbo la Serengeti, Mhe. Jeremiah Mrimi Amsabi, amekabidhi gari la wagonjwa kwa Kituo cha Afya Iramba kilichopo Kata ya Kenyamonta, Wilaya ya Serengeti. Gari hilo linatarajiwa kuboresha huduma za afya kwa wakazi wa Kenyamonta na maeneo ya jirani.
Akizungumza wakati wa hafla ya makabidhiano iliyofanyika katika Kituo cha Afya Iramba, Mhe. Amsabi amewahimiza wananchi kuhakikisha wanatunza gari hilo na kulitumia kwa shughuli za afya pekee. Ameeleza kuwa gari hilo ni sehemu ya jitihada za kuboresha huduma za afya katika jamii.
Kwa upande wake, Mganga Mkuu wa Wilaya ya Serengeti, kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya hiyo, Dkt. Lusubilo Adam, ameahidi kusimamia matumizi sahihi ya gari hilo. Aidha, ametoa shukrani kwa Serikali kwa kuendelea kuwekeza katika sekta ya afya wilayani Serengeti.
Wananchi wa Kata ya Kenyamonta wameishukuru Serikali kwa kuwapatia gari la wagonjwa, wakisema kuwa hatua hiyo itaondoa changamoto kubwa ya usafiri kwa wagonjwa, hususan wanawake wajawazito. Wameeleza kuwa gari hilo litasaidia kuokoa maisha kwa kuhakikisha wagonjwa wanapata huduma za dharura kwa haraka.
Hatua hii ni sehemu ya jitihada za Serikali kuboresha sekta ya afya kwa kuwafikia wananchi katika maeneo yote ya nchi.