WATANZANIA wa madhehebu mbalimbali ya dini wamehimizwa kutenda mema kwa watoto yatima na jamii yenye uhitaji ili Mwenyezi Mungu awepo nao wakati wa changamoto.
Rai hii imetolewa na Askofu Dk. Charles Sekelwa,leo katika hafla ya chakula cha pamoja na watoto yatima,iliyoandaliwa na BAKWATA Mkoa wa Mwanza kwa kushirikiana na kampuni ya The Rock Solution katika kuadhimisha mwaka mpya 2025.
Amesema Sheikh Hasani Kabeke na kampuni ya The Rock Solution wameonesha jitihada kubwa za kusaidia yatima na watu walioko katika mazingira magumu pia, inaonesha juhudi kubwa za kijamii na kidini zinazofanywa na viongozi wa dini.
Askofu Dk.Sekelwa amesisitiza kuwa dini ya kweli isiyo na taka, inazungumzia upendo na huruma, inajali yatima na wajane, na yeyote anayewasaidia wanyonge, Mungu atamkumbuka na kumjibu wakati wa shida ikiwemo ugonjwa .
“Dini ya kweli isiyo na taka inatufundisha kuwajali wanyonge na yatima, kwani kufanya hivyo kunamfanya Mungu kuwa karibu na mtu. Katika Methali 19:17, inasema kwamba msaada kwa maskini unamkopesha Mungu, na hivyo Mungu atajibu kwa njia mbalimbali, hata wakati wa shida,”amesema.
Mwenyekiti Mwenza huyo wa Kamati ya Amani ya Viongozi wa Dini amesema,matendo mema tunayofanya kwa yatima na kuwasaidia wanyonge wenye kuhitaji ni kumkopesha Mungu, ambaye hujibu kwa namna nzuri kwa kupitia njia mbalimbali.
Kwa upande wake, Sheikh Hasani Kabeke amezungumzia umuhimu wa kulea yatima kuwa ni namna nzuri ya kurudisha utamaduni wa zamani ambapo jamii nzima ilishirikiana kuwatunza watoto wa ndugu zao waliopoteza wazazi.
“Kulea yatima sio suala la dini tu, bali ni suala la utu na utamaduni, zamani yatima walilelewa katika familia na jamii nzima ilikuwa na jukumu la kuhakikisha wanalelewa vyema. Hii ilikuwa ni sehemu ya utamaduni wetu, ambapo watoto yatima walikuwa na familia pana ya kuwalea,”amesema.
Sheikh Kabeke amesema, kwa umoja wa Watanzania katika kuwajali na kuwalea watoto yatima, turejee katika utamaduni wa kulea watoto wa ndugu zetu waliopoteza wazazi,badala ya kuishia kwenye vituo au mitaani kama ilivyo leo.
Amesema tukio hilo la chakula cha pamoja linaonesha msukumo kijamii na kidini wa kuwajali yatima, kulinda utamaduni wa kulea watoto wa ndugu na kuhakikisha kuwa wanapata huduma za msingi kama elimu na chakula.
“Nitoe wito wa pamoja kwa Watanzania wenye uwezo kuungana ili kusaidia watoto hawa ili waishi kwa furaha na kufikia malengo yao ya maisha.Ni muhimu kuhakikisha yatima hawa wanapata huduma za kimsingi na maisha bora,”amesema Sheikh Kabeke.
Amewahimiza Watanzania kurudi katika utamaduni wa kulea yatima ili wasijihisi kuwapoteza wazazi wao, bali wahisi kupendwa na kuthaminiwa.
Naye Mjumbe wa Bodi ya The Rock Solution,Dr.Benard Desderius, amesema kampuni hiyo imedhamiria na itaendelea kuhakikisha yatima na watoto wanaoishi katika mazingira magumu wanapata furaha na fursa ya kufikia malengo yao na kutimiza ndoto zao.
Amesisitiza umuhimu wa jamii kushiriki katika kusaidia watoto yatima, kwani kuwekeza kwao ni ibada njema na njia ya kuhakikisha wanakuwa katika maadili bora.