Na Mwamvua Mwinyi,
Desemba 29, 2024
Wanandoa wameaswa kuwa wavumilivu na waaminifu kwenye ndoa zao ili kupunguza wimbi la migogoro ya ndoa, ambayo inaendelea kushika kasi ndani ya jamii.
Rai hiyo imetolewa na Vicar General (Msaidizi wa Askofu) Padre Deogratius Matiika, wakati wa Ibada ya Misa Takatifu ya Kumbukumbu ya kifo cha Baba Mzazi wa Mbunge wa Kibaha Mjini, Silvestry Koka, iliyofanyika huko Mamba Mkolowony, Moshi, mkoani Kilimanjaro, tukio ambalo liliambatana na sherehe za kutimiza miaka 30 ya ndoa ya Mbunge huyo.
Padre Matiika alisema kuwa migogoro ya ndoa ni mingi, lakini wanandoa wanapaswa kukubali mapenzi ya Mungu na kuyakabili kwa uvumilivu.
“Niwangapi tunakumbuka kushukuru Mungu? Kila jambo ni jaribu, na ni lazima tukabiliane nayo kwa kumkimbilia Mungu ili kubariki ndoa na maisha ya wanadamu,” alisisitiza.
Aidha, aliwataka wanajamii kuwajali na kuwapenda wazazi wao, huku akiwahimiza kuwatii na kuwaheshimu.
“Tuwasaidie wazazi, tuwatunze wakiwa hai, tuwaombee wawe na afya njema. Tuwaheshimu kwa sababu mzazi ni kama Mungu hapa duniani,” aliongeza.
Nae mbunge wa Kibaha Mjini, Silvestry Koka, alisema marehemu baba yake alikuwa mtu aliyethamini kumtukuza Mungu.
Aliwashukuru viongozi wa chama na serikali, wanachama wa CCM, na wananchi wote walioshiriki kumbukumbu hiyo, pamoja na sherehe za kutimiza miaka 30 ya ndoa yake na mkewe, Selina Koka.
“Namshukuru Mungu kwa neema alizotujalia kufanikisha miaka 30 ya ndoa, Pia namshukuru mke wangu kwa kunijali na kunitunza kwa upendo,” alisisitiza Koka.
Kwa upande wake Mama Selina Koka alieleza Mungu ni mwema kila wakati, na anamshukuru kwa kila hatua ya maisha yao.
Alisisitiza umuhimu wa mshikamano na upendo katika jamii.
“Tunashukuru umoja ulioonyeshwa na jamii, Ushirikiano huu hauimarishi tu mahusiano, bali pia unajenga upendo na mshikamano.”
Kwa mujibu wa mama Koka , Familia inaahidi kuendelea kushirikiana na viongozi, wanachama wa CCM, na wananchi wote wa Kibaha katika shida na raha.