Naibu waziri ofisi ya Rais utumishi na utawala bora Deus Clement Sangu wakati akizungumza katika kongamano la maadhimisho ya miaka 50 ya kuundwa kwa mkoa wa Rukwa
Baadhi ya machifu wa mkoa wa Rukwa walioshiriki katika maadhimisho ya miaka 50 ya kuundwa kwa mkoa wa Rukwa
Baadhi ya viongozi wa Serikali na Chama waliohudhuria katika kongamano hilo.
…………………..
Neema Mtuka Sumbawanga
Historia ya mkoa wa Rukwa.
Rukwa:Mkoa wa Rukwa ulianzishwa mwaka 1974 kwa kumega sehemu ya mkoa wa Tabora (Mpanda ) na Mbeya (Sumbawanga).
Mnamo mwezi julai 2010 Serikali ya awamu ya nne iliridhia kugawanywa kwa mkoa wa Rukwa na kuanzishwa kwa mkoa mpya wa Katavi.
Mkoa wa Rukwa ni miongoni mwa mikoa 31 ya Tanzania bara unaopatikana Nyanda za juu kusini mwa Tanzania ambao makao yake makuu ni wilaya ya Sumbawanga mjini.
Jina la Sumbawanga zamani sumbu_wanga lilianza kutumika baada ya kuhakikisha unatupa vitu vibaya uchawi na kuingia Sumbawanga ukiwa msafi.
Na ilikuwa inaitwa wilaya ya ufipa yenye himaya 4 hadi ulipopatikana uhuru wa Tanganyika mwaka 1961 na kuwa wilaya ya Sumbawanga.
Mkoa wa Rukwa una jumla ya makabila 7 Wamambwe ,warungu,wanyika/wanyiha,wasukumaa,wakwa,wanyamwanga na wafipa ambalo ndio kabila kubwa na Kuna jumla ya koo 98.
Chakula kikuu cha makabila hayo ni ugali wa ulezi , nyama za porini ,mbogamboga ,panya na uyoga kabla ya kugunduliwa kwa vyakula vingine kama ugali wa mahindi na mpunga.
Mkoa umeundwa na jumla ya wilaya tatu ambazo ni wilaya ya Sumbawanga,wilaya ya Nkasi,na wilaya ya Kalambo.
Katika wilaya zote tatu Kuna jumla ya kata 97 zinazounda mkoa wa Rukwa zenye jumla ya wakaazi 1,540,519 ambapo wanawake 797400 na wanaume ni 743,119 kwa mujibu wa sensa ya watu na makazi iliyofanyika mwaka 2022.
Mkoa huu umepakana na Mkoa wa Katavi, Tabora na Kigoma upande wa kaskazini na Songwe na Mbeya upande wa kusini mashariki.
Aidha unapakana na nchi jirani ya Zambia upande wa kusini na Jamhuri ya kidemokrasia ya Kongo upande wa Magharibi.
mkoa huu upo kati ya Latitudo 7 – 9 kusini ya Ikweta na 30-32 mashariki ya Griniwichi.
Uchumi wa wakazi wa mkoa wa Rukwa.
Kiuchumi wakazi wa mkoa wa Rukwa wanajishughulisha na kilimo cha mazao ya chakula na biashara,ufugaji ,sekta ya utalii ,madini ,uvuvi ,viwanda vidogo pamoja na biashara.
Shughuli kuu ya kiuchumi ni kilimo ambapo mazao ya chakula yanayolimwa kwa wingi ni mahindi ,mpunga viazi vitamu,viazi mviringo,mihogo,maharage na ulezi.
Mazao ya biashara yanayolimwa kwa wingi ni alizeti,ngano ,ufuta na mchikichi.
Pia ziada ya mazao ya chakula kama mahindi,mpunga ,maharage,ulezi ,ngano na karanga hutumika kama mazao ya biashara.
Ufugaji unabaki kuwa shughuli kuu ya pili ya Uchumi katika mkoa wa Rukwa.
Mifugo inayofugwa kwa wingi ni ng’ombe,mbuzi,nguruwe,kondoo,punda,na kuku kwa wakazi wengi shughuli hizi zimebaki katika ngazi ya kujikimu.
Taasisi ya JUMARU ilisajiliwa chini ya Sheria ya mashirika yasiyo ya kiserikali nambari 24 ya mwaka 2002 na marekebisho yake mwaka 2005 nambari 11na 2019 nambari 3.
Taasisi ilianzishwa na kusajiliwa rasmi mwaka 2013 na kupatiwa cheti Cha usajili namba S.A.18941 na wizara ya mambo ya ndani ya nchi.
JUMARU ilizinduliwa na aliyekuwa mkuu wa mkoa wa Rukwa mh.mhandisi Stella Martin Manyanya (Mb) tarehe 20/12 /2013 Sumbawanga.
Taasisi hiyo inajihusisha na mambo mbalimbali ya maendeleo yahusuyo raia wanaoishi ndani na nje ya mkoa wa Rukwa.
Lengo ni kuchagiza maendeleo ya Taifa kwa ujumla katika nyanja za Uchumi,siasa Jamii na utamaduni ambapo taasisi inafanya kazi na makao yake makuu yakiwa ni manispaa ya Sumbawanga.
Kwa kutambua umuhimu wa maendeleo taasisi ya JUMARU kwa kushirikiana na Serikali ya mkoa kupitia kamati ya maandalizi ya maadhimisho ya miaka 50 iliyoundwa na uongozi wa mkoa wameandaa maadhimisho hayo kwa lengo la kukutana na kujadiliana kwa pamoja mustakabali wa mkoa wa Rukwa.
Taasisi ya JUMARU inaendelea kudumisha mahusiano mazuri kati yake na taasisi nyingine na Serikali kwani haina mlengo wowote wa kisiasa wala kukinzana na juhudi zinazofanywana Serikali katika kuleta maendeleo kwa mkoa wa Rukwa.
Tangu kuanzishwa kwa taasisi hiyo imefanikiwa kupata eneo la ekari 70 katika kata ya Pito na kuzitoa kwa ajili ya ujenzi wa chuo cha ualimu Sumbawanga kwa lengo la kuunga mkono jitihada za kuboresha elimu ndani ya mkoa.
Pia kufanya maadhimisho ya miaka 40 kwa kushirikiana na Serikali ya mkoa mwaka 2014.
Kaimu katibu tawala mkoa wa Rukwa David Sebiga amesema Rukwa itajengwa na wanarukwa wenyewe kwa kujitoa na kujituma.
Awali akimkaribisha mgeni rasmi Naibu waziri,ofisi ya Rais utumishi na utawala bora kaimu katibu tawala mkoa wa Rukwa Mhandisi David Sebiga amesema Serikali ya mkoa itahakikisha inashirikiana na wadau mbalimbali wa maendeleo ili kuongeza tija na ufanisi mkubwa katika kukuza maendeleo ya kiuchumi kwa mkoa wa Rukwa.
Akizungumza leo Desemba 28 katika maadhimisho ya miaka 50 ya mkoa wa Rukwa Naibu waziri Sangu amewahimiza wanarukwa walioko nje ya mkoa huo kuwekeza zaidi nyumbani kwao na kuacha tabia ya kukataa walikotoka.
Naibu waziri Sangu amesema Kuna Kila sababu ya wanarukwa kuwekeza nyumbani kwa manufaa ya kizazi cha Sasa na baadae.
Sangu amesisitiza kuwa ni wajibu wa Kila mwanarukwa kuwekeza nyumbani ili kujiepusha na wawekezaji madarali ambao wanaunyonya mkoa wa Rukwa.
“Tuwekeze nyumbani kwa manufaa yetu tuache kujenga nje ambako tunawanufaisha wengine wakati nyumbani kunadorora”. amesema Sangu.
Mwenyekiti wa jukwaa la maendeleo mkoa wa Rukwa (JUMARU) Mwl Helena Khamsini amesema haikuwa rahisi kuandaa kongamano hilo lakini lengo lao la kujiimarisha kiuchumi na kujikomboa kielimu limefanikiwa kwa kiasi kikubwa.
Khamsini amesema taasisi hiyo inaendeshwa kwa mfumo wa mashirika yasiyo ya kiserikali ,hivyo wameandaa mpango kazi wa muda mfupi na muda mrefu unaolenga kuleta mabadiliko ya wanarukwa katika nyanja zote za kiuchumi na kushirikiana kwa ukaribu na Serikali.
Akizungumza katika kongamano hilo mdau wa elimu ngazi ya jamii Samson Simtowe amesema katika kipindi cha miaka 50 ya kuundwa mkoa wa Rukwa mafanikio ya elimu ni makubwa ambapo amesema hapo zamani kulikuwa na shule Moja ya Kantalamba Sekondari ambayo ulianzishwa mwaka 68 lakini hivi sasa Kuna shule nyingi kwenye Kila kata.
Amesema jumla ya wanafunzi 3168 kati ya 46721 mwaka 2020 waliacha shule kwa sababu mbalimbali akiwemo utoro.
Maiko Kachoma mkurugenzi wa Halmashauri ya Busega ambaye pia ni mzaliwa wa mkoa wa Rukwa amesema ni muhimu kwa wanarukwa kujenga nyumbani ambapo amechangia vitendeea kazi kama laptop 2 na sh 1,200,000 kwa ajili ya jukwaa la maendeleo mkoa wa Rukwa ili kujiendesha kiofisi.
Amesema mkoa wa Rukwa una rasilimali nyingi ambazo zikitumika vizuri zinaweza kuwainua wananchi kiuchumi.
Naye mkuu wa wilaya ya Butiama DC Kaegele ambaye ni mzaliwa wa mkoa wa Rukwa amesema amekuja kuungana na wanarukwa ili kuhakikisha mkoa huo unakuwa kimaendeleo.
Amesema mkoa huo unahitaji kupata maendeleo makubwa ambayo yatategemewa na wanarukwa wenyewe kwa kujitoa na kujituma ili kuweza kujiinua kiuchumi na kufanya biashara.
Mzee maarufu Zeno Nkoswe ambaye alishuhudia tukio la kuanzishwa kwa mkoa wa Rukwa amesema baba wa Taifa hili Mwl Julius Kambarage Nyerere alipata sera mpya ya vijiji vya ujamaa katika kata ya Matai Halmashauri ya Kalambo.
Kwa upande wake chifu wa kabila la kifipa chifu Kapufi amesema majukwaa kama hayo yakitumika ipasavyo yatasaidia wananchi kujiinua kiuchumi kwani wanakutana na watu mbalimbali na kupata mawazo mapya.
“Ili kufikia malengo endelevu ya maendeleo Kila mmoja ashiriki Moja kwa Moja katika kuhakikisha anajitoa kwa hali na mali”.
Pia ameitaka Jamii kuendelea kuitunza amani iliyopo na kuendeleza mema yaliyotengenezwa na waasisi wa Taifa.
Mdau wa maendeleo mkoa wa Rukwa Jackline Mzindakaya amesema ni wakati wa wanarukwa kuchangamkia fursa zinazojitokeza kwenye maeneo yao na kuhakikisha kuwa wanashiriki kikamilifu.
Kilele cha maadhimisho hayo yametanguliwa na matukio mbalimbali ikiwemo utoaji wa elimu ya uzalendo kwa wakazi wa mkoa wa Rukwa kupitia vyombo mbalimbali vya habari.
Sambamba na hilo pia zoezi la upandaji wa Miche 6000 ya miti yenye mchanganyiko wa miti ya mbao,kivuli ,matunda na na miti ya urembo katika shule ya Sekondari ya Kantalamba kwa lengo la kuhamasisha matumizi ya nishati safi kwa ajili ya kutunza na kuhifadhi mazingira.