TAARIFA KWA UMMA
Jeshi la Polisi limejipanga vizuri kuimarisha usalama katika sikukuu za Christimas na Mwaka mpya kwa kushirikiana na Wananchi, Viongozi wa Nyumba za Ibada, Kamati za Usalama za Nyumba za Ibada ambako Ibada mbalimbali zitafanyika na Viongozi wa Serikali za Mitaa ili kuhakikisha kila mmoja anasheherekea kwa amani na utulivu.
Aidha, Jeshi la Polisi linatoa wito kwa kila mmoja wetu ili usheherekee na kufanya shughuli zako katika mazingira ya amani, utulivu na usalama katika kipindi hiki cha Sikukuu za mwisho wa Mwaka, tukumbuke usalama unaanza na wewe mwenyewe kwa kujiepusha na vitendo vitakavyo hatarisha usalama wako, mali zako na familia yako.
Vitendo kama vile kuacha nyumba bila uangalizi, kutumia vilevi kupindukia, kuacha watoto wakizurura hovyo bila uangalizi wa mtu mzima na mwenye akili timamu. Tuepuke kuweka mali au fedha katika hali hatarishi.
Aidha, kuhusiana na hatua za kuzuia ajali pamoja na kwamba ukamataji wa wanaovunja sheria za usalama barabarani unaendelea sambamba na utoaji elimu, tunatoa wito kwa kila mmoja wetu kukemeana papo kwa papo pamoja na kutoa taarifa pale tunapoona mwenzetu anafanya vitendo vya kizembe na vile vinavyohatarisha usalama wa maisha yetu barabarani. Baadhi ya ajali zilizotokea ukisikiliza mashuhuda inaonyesha wazi tungekuwa na utamaduni na uthubutu wa kukemeana zingeepukika hata kwa yale magari yaliyokuwa yanatumiwa na familia na mengineyo.
Pia, Jeshi la Polisi linatoa wito tuendelelee kushirikiana katika vikao vya ngazi ya familia, mitaa, nyumba za ibada pamoja na makatazo ya Mwenyezi Mungu nini chanzo cha uhalifu ili tuweze kuwa na mikakati ya pamoja ya kuvizuia ikiwepo malezi bora.