Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko, akihutubia wananchi (hawapo pichani) , leo wa Magu katika Uwanja wa Mwanankanda, na kuwahimiza kutumia nishati safi ya kupikia.
*ASILIMAI 99 YA VIJIJI VYAFIKISHIWA UMEME MAGU
*MAJIKO YA GESI 3,255 KUSAMBAZWA KWA BEI YA RUZUKU MAGU
NA BALTAZAR MASHAKA,MAGU
SERIKALI imetenga zaidi ya sh.milioni 600 za kupeleka umeme jua katika Kisiwa cha Ijinga wilayani Magu,huku ikiwaahakikishia maendeleo wananchi wa wilaya hiyo.
Kauli hiyo ilitolewa jana na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati,Dkt.Doto Biteko,wakati akihutubia Mkutano Mkuu wa CCM Jimbo la Magu,wa uwasilishaji wa taarifa ya utekelezaji wa ilani ya uchaguzi.
Amesema Kijiji cha Ijinga ni kisiwa kilichopo ndani ya Ziwa Victoria, ndicho pekee kilichosalia kufikishiwa umeme wilayani humo, hivyo kitafikiwa na huduma hiyo baada ya serikali kutenga sh. milioni 619 ambapo mkandarasi Master Volt yupo eneo la mradi.
“Mnavijiji 82 ambapo vijiji 81 vyote vina umeme kimebaki kijiji kimoja kipo kwenye kisiwa,tuliona itachukua muda kuwapelekea umeme kwa kulaza nyaya (cable)chini ya maji,watu wa Ijinga ni Watanzania wanastahili kupata umeme, tumetenga milioni 619 ili nao wapate umeme,” amesema
Dk.Biteko amesema fedha hizo zitatumika kupeleka umeme jua (solar) kwa wananchi wa kisiwa cha Ijinga,kwamba kazi ya serikali iliyobaki ni kupeleka maendeleo kwa wananchi na kuwataka washirikiane kuijenga Magu.
Kwa upande wake Mbunge wa Magu (CCM),Boniventura Kiswaga amemshukuru Rais Dk.Samia Suluhu Hassan kwa kufikisha umeme katika vijiji 81 kati ya 82 jimboni humo huku akisema kazi kubwa imefanyika, umeme sasa ufikia asilimia 99 vijijini.
“Nilipochaguliwa kuwa mbunge ni vijiji 22 tu vilikuwa na umeme kati ya 82,tumebakiza kijiji kimoja tu cha Ijinga kuna mpango wa kuweka cable ili kufikisha umeme kisiwani humo, sasa kazi iliyobaki ni kufikisha nishati hiyo katika vitongoji,”alisema.
Amemshukuru Dk. Rais Samia kwa kuibeba ajenda ya Nishati Safi ya kupikia ambayo itasaidia kuokoa afya za wananchi na mazingira huku akiipongeza REA kwa kuibeba ajenda hiyo ya Mhe.Rais kwa kuandaa programu mbalimbali ikiwemo ya usambazaji wa majiko ya gesi kwa bei ya asilimia 50 ya ruzuku.
Naye Msimamizi wa Miradi Mkoa wa Mwanza, Mhandisi Awesa Rashid,amesema Wakala wa Usambazaji Umeme Vijijini (REA),unatekeleza miradi ya kusambaza umeme mkoani humo baada ya kukamilisha kusambaza umeme vijijini,awamu inayofuata sasa ni kwa vitongoji.
“Tunatekeleza mradi wa kusambaza umeme katika vitongoji 15 kwa kila Jimbo ikiwemo Jimbo la Magu, kwa sasa mradi huu unaendelea kote nchini,” amefafanua na kutoa wito kwa wananchi kuchangamkia fursa ya kuunganishiwa umeme kwa bei ya sh. 27,000 tu ili kujiletea maendeleo.
Aidha, kuhusu utekelezaji wa Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia 2024-2034, Mhandisi wa Miradi wa REA,Ramadhani Mganga amesema wakala huo umeendelea kuhamasisha wananchi kutumia bidhaa za nishati safi za kupikia ili kuepukana adha mbalimbali zinazosababishwa na matumizi ya nishati zisizo safi.
“Tumuunge mkono Mhe. Rais Dk.Samia ili kuhakikisha ifikapo mwaka 2034, asilimia 80 ya Watanzania wawe wanatumia nishati,” amesema Mhandisi Mganga na kuongeza kuwa, upande wa Mkoa wa Mwanza jumla ya majiko 19,530 yatasambazwa,kila wilaya itapata majiko 3,255 kwa bei ya ruzuku ya asilimia 50.
“Tupo hapa kutoa elimu na kuhamasisha wananchi kutumia nishati safi. Napenda kuwahimiza wananchi wanapokwenda kununua mtungi huu wa ruzuku ni lazima uwe na kitambulisho cha Taifa,” amesisitiza.
Kwa nyakati tofauti wananchi waliipongeza serikali kupitia REA kwa kuendelea kuwa mstari wa mbele katika suala la matumizi ya nishati safi.
“Mpango huu wa serikali tumeupokea vizuri.Tunamshukuru Rais wetu Dk. Samia Suluhu Hassan,ameturahisishia Watanzania kuepuka uharibifu wa mazingira,ili kupata kuni na mkaaa tulikuwa tunakata miti ovyo, madhara yake sasa tunayaona,” alisema Njile Ng’washi,Mkazi wa Itumbili, Magu.