Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
KAMPUNI ya mawasiliano ya Yas Tanzania imezindua kampeni ya ‘Magifti ya Viwango’ itakayodumu kwa miezi mitatu katika msimu huu wa sikukuu, ikiwa na zawadi mbalimbali kwa wateja wake, ikiwemo gari jipya lenye thamani ya Sh milioni 100, Sh milioni moja kila siku, simu janja aina ya iPhone 18 kila wiki na Sh milioni 10 kila mwezi.
Kampeni hiyo iliyozinduliwa Novemba 17, 2026, inalenga kusherehekea Mwaka wa Viwango pamoja na kuwashukuru wateja walioendelea kuiamini kampuni hiyo na kutumia huduma zake, sambamba na mafanikio yaliyopatikana katika kuimarisha mtandao wake nchini.
Katika kipindi hicho, Yas imewekeza katika kupanua wigo wa mtandao, kuongeza uwezo wake na kuimarisha uthabiti wa huduma, hatua zilizoifanya kampuni hiyo kujivunia mtandao wenye kasi zaidi na unaofika katika maeneo mengi zaidi nchini.
Kwa mujibu wa kampuni hiyo, mtandao wake una zaidi ya minara 4,900 huku teknolojia ya 5G ikiendelea kupanuliwa sambamba na teknolojia mpya za mawasiliano ikiwemo VoLTE, zinazowawezesha watu binafsi, wafanyabiashara na taasisi kushiriki kikamilifu katika uchumi wa kidijitali.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa kampeni hiyo, Afisa Mkuu wa Teknolojia na Ufundi wa Yas Tanzania, Emmanuel Mallya, alisema kampuni hiyo imewekeza zaidi ya Sh trilioni 1.2 katika mtandao wake kwa lengo la kuwapatia Watanzania huduma bora za mawasiliano.
Alisema uwekezaji huo umewezesha kampuni kuendelea kupanua wigo wa mtandao, kuongeza uwezo wake na kuimarisha uthabiti ili kuwawezesha wateja kufanya shughuli mbalimbali kupitia teknolojia, ikiwemo kupiga simu, kutazama maudhui mtandaoni, kujifunza, kufanya kazi na kuendesha biashara.
“Uwekezaji wetu wa zaidi ya shilingi trilioni 1.2 kwenye mtandao unadhihirisha dhamira yetu ya kuwapatia Watanzania huduma bora za mawasiliano. Tunataka kuhakikisha mtandao wetu unarahisisha shughuli zao za kila siku,” alisema Mallya.
Kwa upande wake, Afisa Mkuu wa Biashara wa Yas Tanzania, Norman Kiondo, alisema mtandao imara na wa kisasa una mchango mkubwa katika kuharakisha mageuzi ya kidijitali, kuongeza ushindani wa biashara na kuchochea ukuaji wa uchumi.
Alisema wakati Tanzania ikiendelea kushuhudia biashara nyingi zikikumbatia teknolojia ya kidijitali kwa ajili ya kukuza shughuli zao na kutengeneza fursa mpya, Yas inalenga kutoa siyo tu mtandao unaowezesha uchumi wa kidijitali, bali pia suluhisho za kidijitali zitakazosaidia biashara kujiendesha kwa ufanisi na kukua.
“Tunaposherehekea Mwaka wa Viwango, biashara nyingi zaidi nchini zinakumbatia teknolojia ya kidijitali ili kukua na kutengeneza fursa mpya. Lengo letu si tu kutoa mtandao unaoendesha uchumi wa kidijitali, bali pia kutoa suluhisho za kidijitali zitakazosaidia biashara kujiendesha kwa ufanisi na kukua,” alisema Kiondo.
Alisema uwekezaji unaoendelea kufanywa na kampuni hiyo unafungua fursa mbalimbali nchini, huku akisisitiza kuwa mafanikio yaliyopatikana katika Mwaka wa Viwango yasingewezekana bila mchango wa wateja walioendelea kuiamini na kutumia huduma zake.
Naye Mkurugenzi wa Huduma kwa Wateja wa Yas Tanzania, Mwangaza Matotola, alisema kampeni ya Magifti ya Viwango ni sehemu ya utamaduni wa kampuni hiyo wa kuwathamini na kuwazawadia wateja wake, ambao kwa sasa wamefikia zaidi ya milioni 34.
Alisema kampeni hiyo ni njia ya kuwashukuru wateja kwa imani yao na kuwa sehemu ya safari ya ukuaji wa kampuni, huku ikilenga kuwapa furaha wakati wa kumaliza mwaka na kuwapa matumaini wanapoanza mwaka mpya.
“Magifti ya Viwango ni njia yetu ya kuwashukuru wateja wetu kwa kutuamini na kuwa sehemu ya safari yetu ya ukuaji. Wateja wetu ndio kiini cha Mwaka wa Viwango, na kupitia kampeni hii tunasherehekea pamoja nao,” alisema Matotola.
Aliongeza kuwa zawadi zilizotolewa katika kampeni hiyo zimezingatia mahitaji halisi ya kila siku ya wateja, zikiwemo kusaidia wafanyabiashara wadogo kukuza mitaji yao na familia kukabiliana na gharama mbalimbali, hususan mwanzoni mwa mwaka.
Alisema kwa mfanyabiashara mdogo, fedha taslimu zinaweza kuwa mtaji wa kukuza biashara, huku kwa familia zikiweza kusaidia kugharamia mahitaji ya nyumbani na gharama za watoto kurejea shuleni, wakati mshindi wa gari atapata fursa ya kuboresha maisha yake.
Kupitia kampeni hiyo, wateja watapata nafasi ya kujishindia Sh milioni moja kila siku, simu janja aina ya iPhone 18 kila wiki na Sh milioni 10 kila mwezi. Aidha, kutakuwa na zawadi maalumu za sikukuu za fedha taslimu za Sh milioni 10 na Sh milioni tano, huku zawadi kuu ikiwa ni gari jipya lenye thamani ya Sh milioni 100.
Akifafanua namna ya kushiriki, Matotola alisema kila mteja atakayenunua kifurushi kupitia Yas App, kwa kubonyeza \*147\*00# au kupitia huduma ya Yas Rusha atapata nafasi ya kuingia katika droo ya ushindi.
Alisema wateja pia wataongeza nafasi zao za kushinda kwa kulipia bili za huduma ya intaneti ya Fiber, kufanya marejesho ya mikopo ya ununuzi wa vifaa, pamoja na kupakua na kujisajili katika Yas App.
“Tunataka wateja wetu waendelee kufurahia huduma wanazotumia kila siku huku wakipata fursa ya kujishindia zawadi kabambe. Kadiri mteja atakavyofanya manunuzi na malipo mengi zaidi, ndivyo atakavyoongeza nafasi yake ya kushinda,” alisema.
Kwa upande wake, Japhet Mwaikenda, mteja wa Yas anayeishi Dar es Salaam, alisema zawadi za fedha taslimu zitakuwa msaada mkubwa kwa familia katika kukabiliana na majukumu ya kifedha yanayoongezeka mwanzoni mwa mwaka.
Alisema mwezi Januari huwa na gharama mbalimbali kwa familia, zikiwemo ada za shule na mahitaji mengine ya nyumbani, hivyo kujishindia Sh milioni moja kutakuwa msaada mkubwa kwake.
“Mwezi Januari huwa na majukumu mengi ya kifedha, yakiwemo kulipa ada za shule na kugharamia mahitaji mengine ya familia. Hivyo, kujishindia shilingi milioni moja kutakuwa msaada mkubwa kwa familia yangu,” alisema Mwaikenda.
Aliongeza kuwa kwa kuwa tayari hununua vifurushi kwa ajili ya kupiga simu na kutumia intaneti, kupata nafasi ya kushinda zawadi kupitia manunuzi hayo ni motisha ya ziada kwake.
