katikati ni Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Brigedia Jenerali Ahmed Abbas Ahmed akikata utepe kuzindua kampeni ya ugawaji vyandarua mkoani Ruvuma

 Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma kulia Brigedia Jenerali Ahmed Abbas Ahmed akimkabidhi chandarua mzee Jacob Luambano mkazi wa Manispaa ya Songea

……..

Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Brigedia Jenerali Ahmed Abbas Ahmed amezindua rasmi kampeni ya usambazaji na ugawaji wa vyandarua bure kwa wananchi wa mkoa huo, ikiwa ni mkakati wa kufikia lengo la kutokomeza malaria nchini (Zero Malaria) ifikapo mwaka 2030.

Akizungumza katika hafla ya uzinduzi huo, Brigedia Jenerali Ahmed amesema kiwango cha maambukizi ya malaria mkoani Ruvuma bado kiko juu ya wastani wa kitaifa, hali inayolazimu kuongeza kasi ya mapambano dhidi ya ugonjwa huo.

Pamoja na mambo mengine, RC Ahmed amekemea tabia ya baadhi ya wananchi kutumia vyandarua kinyume na malengo, ikiwemo kuvitumia kuvulia samaki na kuzungushia bustani za mbogamboga.

Pia, ametoa wito kwa wananchi wa maeneo ya mijini na vijijini kuzingatia usafi wa mazingira, kudhibiti mazalia ya mbu kwa kutumia viuatilifu vya kuua viluilui, pamoja na kuacha matumizi holela ya dawa bila kupima ili kujua ugonjwa halisi.

Naye Katibu Tawala wa Mkoa wa Ruvuma, Wakili Mary Makondo, amesema kulinda afya za wananchi ni msingi muhimu wa kuwa na nguvu kazi imara itakayochangia ukuaji wa pato la kaya na taifa kwa ujumla.

Kwa upande wake, Mwakilishi wa Bohari ya Dawa (MSD), Mboyi Wishega, amesema vyandarua 901,336 vitasambazwa katika vituo 888 vya kutolea huduma kwenye halmashauri tano za mkoa huo ambazo ni Madaba, Namtumbo, Nyasa, Songea Vijijini na Tunduru.

Kwa upande mwingine, Mwakilishi wa Wizara ya Afya, Peter Gitanya, amesisitiza umuhimu wa kudhibiti vyandarua hivyo visichepushwe kwenda nchi jirani ili malengo ya kitaifa ya kutokomeza malaria yaweze kutimia.

Akitoa Takwimu za ugonjwa wa Malaria za mkoa wa Ruvuma, Mganga Mkuu wa Mkoa Dkt. Louis Chomboko, amesema mkoa umefanikiwa kupunguza kiwango cha maambukizi ya malaria kutoka asilimia 26 mwaka 2007 hadi kufikia asilimia 8.3 sasa.

Mkazi wa Manispaa ya Songea, Jacob Lwambano, ameishukuru serikali kwa kujali afya za wananchi na kuahidi kuwa watavitunza vyandarua hivyo na kuvitumia kwa lengo lililokusudiwa