Na Silivia Amandius, Kagera.
Wananchi wa Mkoa wa Kagera wametakiwa kutumia bidhaa za ndani, zikiwemo kahawa maarufu ya Taifa Coffee, ili kujikinga na madhara mbalimbali ya kiafya, yakiwemo msongo wa mawazo. Wito huu umetolewa wakati wa maonesho ya biashara yanayoendelea katika Tamasha la Ijuka Omuka, lililoandaliwa na Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Mhe. Hajjat Fatma Mwassa, kwa lengo la kuhamasisha uzalendo na uwekezaji wa wazawa wa Kagera walioko ndani na nje ya nchi.
Wakati wa ziara katika banda la Taifa Coffee, lililopo viwanja vya CCM Bukoba, Olestus Saloni, kwa niaba ya mkurugenzi wa kahawa hiyo, aliwahamasisha wananchi kupenda na kutumia bidhaa za nyumbani. Alieleza kuwa Taifa Coffee, inayozalishwa katika kata ya Maruku, Wilaya ya Bukoba, si tu kinywaji chenye ladha ya kipekee bali pia kina faida nyingi kiafya, zikiwemo kupunguza msongo wa mawazo, kuimarisha kumbukumbu, na kusaidia kinga ya mwili dhidi ya maradhi kama saratani ya ini.
“Kahawa hii ina zaidi ya ladha mia saba zinazochangamsha mwili. Pia husaidia kuyeyusha mafuta, kuongeza virutubisho muhimu mwilini, na kuchangamsha akili. Tunatoa wito kwa jamii kuitumia ili kuboresha afya na kuendeleza uchumi wa ndani,” alisema Saloni.
Aidha, Saloni alitoa rai kwa vijana wa Kagera kuwekeza katika viwanda vya ndani na kutumia fursa zilizopo kwa bidii. Aliongeza kuwa kiwanda cha Taifa Coffee, kilichoanzishwa Agosti 2024, ni mfano wa mafanikio ya uwekezaji wa ndani, huku akiwashukuru Rais Samia Suluhu Hassan na uongozi wa Mkoa wa Kagera kwa juhudi zao za kuleta maendeleo katika eneo hilo.
Maonesho hayo yanaendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa bidhaa za ndani na njia za kuzitumia kuboresha maisha yao.