*Aeleza umuhimu wa kuheshimu matakwa ya wananchi katika uongozi
*Agiza mabadiliko kwenye uteuzi wa wagombea na mafunzo kwa viongozi wa Serikali za Mitaa
*Apongeza utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi
Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dkt. Emmanuel John Nchimbi, ameweka msisitizo juu ya umuhimu wa CCM kuendelea kujikita katika kutekeleza mahitaji na matakwa ya wananchi, kama njia ya kudumisha imani ya Watanzania kwa chama hicho.
Akizungumza katika Mkutano Mkuu wa CCM Jimbo la Nzega Mjini, leo Desemba 20, 2024, Balozi Nchimbi alihimiza viongozi wa Chama na Serikali kuhakikisha kila hatua inayochukuliwa inazingatia maslahi ya wananchi. Alisisitiza kuwa CCM ni chama kinachowaheshimu watu na kuhakikisha kila kiongozi anawajibika ipasavyo kwa jamii.
Katika hotuba yake, Balozi Nchimbi alitoa mfano wa uteuzi wa mgombea wa CCM katika Kitongoji cha Mkoga, Wilaya ya Mkuranga, Mkoa wa Pwani, ambapo mgombea aliyeshindwa kukubalika na wananchi aliteuliwa tena. Alielekeza uchaguzi wa kura za maoni urudiwe na mgombea huyo asishiriki, akisisitiza kuwa chama hakiwezi kufanikisha malengo yake bila kuheshimu matakwa ya wananchi.
“Misingi ya CCM ni kuheshimu watu na kuwatumikia. Hatuwezi kuwa chama cha wananchi kama tunapuuzia sauti yao,” alisema Nchimbi.
Pamoja na kutoa maelekezo hayo, Balozi Nchimbi alisisitiza umuhimu wa kuwajengea uwezo viongozi wa Serikali za Mitaa, vijiji, na vitongoji waliochaguliwa hivi karibuni. Alisema mafunzo maalumu yatasaidia kuboresha utekelezaji wa majukumu yao kwa tija na uwajibikaji.
Akizungumzia Jimbo la Nzega Mjini, Balozi Nchimbi aliwapongeza viongozi wa Chama na Serikali kwa utekelezaji mzuri wa Ilani ya Uchaguzi. Pia alisifu mshikamano na umoja uliopo kati ya viongozi na wananchi, ambao umeimarisha imani ya wananchi kwa CCM.
Katika mkutano huo, Balozi Nchimbi pia alizindua ukumbi wa mikutano wa kisasa unaomilikiwa na CCM Wilaya ya Nzega na kugawa pikipiki 229 zilizotolewa na Mbunge wa Nzega Mjini, Mhe. Hussein Mohamed Bashe, kwa viongozi wa Chama na jumuiya zake katika ngazi mbalimbali.
Hotuba ya Balozi Nchimbi imeendelea kuthibitisha kuwa CCM inabaki kuwa chama kinachoweka wananchi mbele katika kila hatua ya maamuzi, kwa kuhakikisha uwajibikaji, ushirikishwaji, na ufanisi wa viongozi katika ngazi zote za uongozi.