Sheikh Hasani Kabeke, akiwaongoza baadhi ya wananchi wa Mkoa wa Kigoma, kutembelea Hifadhi ya Taifa Gombe leo Disemba 20, 2024
………….
NA BALTAZAR MASHAKA,KIGOMA
WAKAZI wa Mkoa wa Kigoma wameaswa kutangaza vivutio vya utalii mkoani humo,ikiwemo Hifadhi ya Taifa ya Gombe,inayojivunia wanyama aina ya sokwe na maporomoko ya maji yenye mandhari ya kuvutia.
Alhaji Sheikh Hasani Kabeke,amesema leo wakati wa kuhitimisha tamasha la kihistoria na utamaduni wa Mji Mkongwe wa Ujiji Kigoma,lililolenga kuutangaza mji huo na vivutio vingi vya utalii mkoani Kigoma.
Amesema mkoa huo umeingia katika historia mpya ya kuandaa tamasha la kwanza la kihistoria na utamaduni wa mji mkongwe wa Ujiji,kuhamasisha na kutangaza vivutio vya utalii,ili kukuza utalii na kuleta maendeleo mkoani humo.
“Tamasha hili ni mwanzo mzuri wa kuhamasisha maendeleo ya kiutalii na kuchochea uchumi wa Mkoa wa Kigoma.Ni matarajio yetu serikali itatuunga mkono na mkurugenzi uwepo wako hapa umetudhihirishia uungwana wa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dk.Samia Suluhu Hassan pia,tunawapongeza Mkuu wa mkoa na mkuu wa wilaya kwa ushirikiano wao,”amesema Sheikh Kabeke.
Amesema tamasha hilo ni heshima kwa wananchi wa Kigoma na halifungamani na chama chochote cha siasa,linahusisha watu wa vyama vyote na kuonya,siasa ikiingizwa halitapiga hatua na kuwataka wanasiasa kupingana kwa kujenga hoja na kunadi sera zao katika majukwaa yao.
Sheikh Kabeke ambaye alikuwa Mwenyekiti wa tamasha hilo,amesema ni jukumu la kila mwanakigoma,kutangaza na kudumisha vivutio vya utalii vya Ujiji na Mkoa wa Kigoma kwa ujumla.
“Mji wa Ujiji una zaidi ya miaka 300,kuna majengo ya ibada na misikiti yenye zaidi ya karne tano,kuna kanisa lenye miaka 100 na visima vilivyochimbwa wakati wa utawala wa Waingereza,” amesema Sheikh Kabeke kwa furaha na kusisitiza umuhimu wa wananchi kuupenda na kuuenzi utamaduni wao pamoja na mji wa Ujiji Kigoma.
Amempongeza Rais Dk.Samia kwa juhudi zake za kushiriki kutangaza vivutio vya utalii,kupitia filamu ya Royal Tour ambayo inalenga kukuza utalii nchini, na katika kuunga mkono juhudi hizo,Kigoma wameamua kuutangaza mji wa kale wa Ujiji,uliojaa mambo ya kihistoria na utamaduni,hata kabla ya ujio wa Dk.Livingstone mwaka 1871.
“Tunampongeza kwa dhati Rais Dk.Samia Suluhu Hassan kwa kutoka Ikulu na kwenda kuigiza Filamu ya Royal Tour ikiwa ni kutangaza vivutio vya utalii nchini,Kigoma tumeamua kumuunga mkono kwa kuutangaza mji wa kale wa Ujiji wenye mambo mengi ya kuvutia,”amesema Sheikh Kabeke.
Ameeleza Mji wa Ujiji ni nyumbani kwa makabila ya Wakusu,Waluba,Wagoma,Wanya,
Kiongozi huyo wa kiroho ameipongeza serikali kwa kuufungua Mkoa wa Kigoma,kupitia ujenzi wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania,Hospitali ya Taifa ya Muhimbili Kigoma,mradi wa umwagiliaji Bonde la Lwiche,barabara za Kibondo na Uvinza za kiwango cha lami,zitarahisisha usafiri na kuchochea maendeleo.
Sheikh Kabeke amesisitiza kudumisha amani,utulivu na umoja,wananchi kuendelea kuwa wamoja bila kujali dini,kama ilivyo kwa viongozi wa madhehebu mbalimbali ya dini,wanaishi kwa umoja na kushirikiana.
Amesema makabila hayo yaendelee kutunza amani,umoja na mshikamano ili kuendeleza utamaduni wa Ujiji na Kigoma,kwani umoja wa wananchi hao utaleta maendeleo endelevu.
“Kwa kushirikiana na serikali,wananchi wa Kigoma wanayo nafasi ya kuendelea kutangaza vivutio vya utalii,kuenzi historia ya mji wao na kuleta maendeleo endelevu kwa mkoa na nchi kwa ujumla,”amesema Sheikh Kabeke.
Katika kilele cha tamasha hilo,tuzo mbalimbali zilitolewa kwa baadhi ya watu waliowahi kutoa michango katika Mkoa na Taifa,akiwemo Sheikh Amri Abeid Kaluta, Mwafrika wa kwanza kuwa Waziri wa Sheria na Waziri wa Utamaduni.
Sheikh Kaluta,alifariki mwaka 1964 akiwa na umri wa miaka 40,ametimiza miaka 100 tangu kuzaliwa huku tamasha hilo likifanikiwa kwa jamii kuonesha umoja na mshikamano katika kutangaza utalii na utamaduni wa Kigoma.