Na Sophia Kingimali.
SEKTA ya habari na Utangazaji nchini imeonesha utayari kuishi katika dhima ya Rais Samia Suluhu Hassan ya 4R kwalengo la kufanya maridhiano,uvumilivu,kuleta mageuzi na ujenzi mpya ili Tanzania izidi kusonga mbele na watanzania wapate yale wanayoyatarajia katika nchi.
Hayo yasemwa leo Disemba 18,2024 jijini Dar es Salaam na Wazuri wa Habari Prof. Kabudi Palamagamba wakati akiongea na wadau wa habari na utangazaji.
Amesema tangu 4R hizo kutangazwa na Rais Samia kumekuwa na ushirikiano mkubwa kati ya Sekta ya habari na wadau wa habari katika masuala yanayohusu kuboresha sera ,sheria na kanuni.
Prof.Kabudi amesema kuongezeka kwa uhuru wa habari na ukuaji wa sekta ya habari nchini ni moja ya mafanikio ya serikali ya awamu ya sita.
”Kuwepo uhuru wa habari nchini ambayo inalindwa na ibara ya 18 ya Katiba ya nchi inayoeleza kila Raia anahaki ya kupata taarifa wakati wowote.
”Kutokana na usimamizi mzuri wa sekta ya habari nch imeweza kupiga hatua kubwa katika kuimarisha uhuru wa habari ambapo kwa Mujibu wa Ripoti ya uhuru wa vyombo vya habari dunia ya mwaka 2024, Tanzania imekuwa ya 57 kwa mwaka huu kutoka 145 kwa mwaka 2023,”amesema.
Amesema taifa lolote linalijitambua kama ilivyo Tanzania lazima iipe sekta ya habari nafasi maalum.
Kwa Upande wake Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa amesema vyombo vya habari zaidi ya 1200 vimesajiliwa na kuajiri makundi mbalimbali ya watu wakiwemo watangazaji na mafundi mitambo.
Msigwa alisema serikali inaendelea kuboresha sekta hiyo ili kuleta mabadiliko chanya kwa kufanya marekebisho ya baadhi ya sheria za habari kwani sekta ya habari imekuwa ikichangia mapato ya serikali kupitia kodi na matangazo na huduma mbalimbali
Naye Katibu Mkuu wa Chama cha Wafanyakazi wa Vyombo vya Habari Tanzania (JOWUTA),Selemani Msuya amemuomba Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Prof. Palamagamba Kabudi kushirikiana na Ofisa ya Waziri Mkuu Ajira, Kazi,Vijana na Watu wenye Ulemavu kuhakikisha Sheria ya ajira na Mahusiano kazini ya mwaka 2004 inatekelezwa kwenye sekta ya habari.
Amesema sekta ya habari ina mchango mkubwa katika maendeleo ya nchi na jamii, ila maslahi ya waandishi wa habari yamesahaulika, hivyo kumuomba Waziri aweke mkazo kwa kushirikiana na ofisi ya Waziri Mkuu Ajira na Kazi.
”Kumekuwepo na kasi kubwa ya kusajili vyombo vya habari, lakini vyombo hivyo havizingatii sheria ya ajira na mahusiano kazini ya mwaka 2004, hali ambayo inasababisha waandishi kuishi katika maisha magumu,”amesema Msuya.
Amesema waandishi wanapaswa kupata bima ya afya, kuchangia kwenye Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), WCF na mingine na hilo haliwezi kukamilika kama hawatapewa mikataba ya ajira kama sheria inavyotaka.
Aidha Msuya ametolea mfano iwapo kuna vyombo vya habari 1,000 na kila chombo kina wafanyakazi 20 na kila mfanyakazi akalipwa shilingi laki nane au milioni 1 na akiwa anapata huduma za bima, NSSF na makato ya mshahara serikali itapata zaidi ya shilingi bilioni 1 kila mwezi.