Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge, Utawala, Katiba na Sheria Mhe. Dkt. Joseph K. Mhagama (Mb) ameongoza ujumbe wa Tanzania katika ziara na mazungumzo baina ya Kamati hiyo na Wawekezaji Diaspora ambao ni Raia wa Nchi Nyingine wenye asili ya Tanzania (Non-Citizen Diaspora) katika Visiwa vya Muungano wa Comoro.
Kwa ujumla kikao hiki kimejadili changamoto na fursa za uwekezaji kupitia diaspora na kushauri mapendekezo yanayolenga kuongeza mchango wa Diaspora katika eneo la Uwekezaji.
Katika kikao hiki, Mwekezaji Bw. Waaadane Said, Diaspora wa Tanzania na Mkurugenzi wa Kampuni ya Sawaprix ameahidi kuwekeza nchini Tanzania ikiwa ni pamoja na kuomba kuunganishwa na wafanyabiashara wa Tanzania ili kuuza bidhaa mbalimbali za Tanzania nchini Comoro.
Itakumbukwa kuwa, Kamati hiyo ipo nchini Comoro kwa ajili ya kujifunza na kadhalika kupata uzoefu wa Nchi hiyo katika kuwashirikisha Diaspora kuchangia maendeleo ya Taifa.