Wizara ya Katiba na Sheria imehitimisha kampeni maalum ya utoaji elimu ya Utawala Bora na Uraia Mkoani Mara, kampeni iliyohusisha ziara katika wilaya zote za mkoa huo. Timu ya wizara ilikutana na kamati za usalama, wakurugenzi, wakuu wa idara mbalimbali za halmashauri, na kutoa mafunzo yaliyolenga kuboresha utendaji kazi na kuimarisha utekelezaji wa majukumu ya kiserikali.
Akizungumza baada ya kukamilisha zoezi hilo, Wakili wa Serikali Mkuu kutoka Wizara ya Katiba na Sheria, Joyce Mushi, alisema kampeni hiyo ilikuwa na lengo la kuwawezesha viongozi na watendaji kuelewa na kufanikisha utekelezaji wa dhana ya 4R za Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.
“Tumeweka mwanga na tumewafungua. Niwaombe viongozi mliopata mafunzo haya, hasa hapa Wilaya ya Bunda ambako tumemalizia kampeni hii, kuyatumia kikamilifu. Hatutarajii kuona mabadiliko hasi baada ya mafunzo haya. Wizara itahakikisha inafuatilia utekelezaji,” alisema Joyce Mushi.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Bunda, Dkt. Vincent Naano, aliishukuru Wizara ya Katiba na Sheria kwa kuleta kampeni hiyo na kusisitiza umuhimu wa kushirikisha watumishi wa ngazi za chini, wakiwemo wenyeviti wa vijiji, makatibu tarafa, na madiwani, ili kuhakikisha mafunzo hayo yanatekelezwa kikamilifu.
“Nazingatieni mafunzo mliyopata na tumieni ujuzi huo kutatua kero za wananchi. Utawala Bora ni nyenzo muhimu ya kupunguza migongano na changamoto katika maeneo yenu ya kazi,” alisema Dkt. Naano.
Mafunzo haya yanatarajiwa kuwa chachu ya maendeleo katika Mkoa wa Mara, huku yakichochea uwajibikaji na uwazi katika utendaji wa viongozi wa serikali.