Disemba 17, 2024
Na Mwamvua Mwinyi, Pwani
WAZIRI wa Viwanda na Biashara, Dkt. Seleman Jafo, amemuagiza Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Dkt. Hashil Abdallah, kuhakikisha kuwa maonyesho ya tano ya viwanda mkoani Pwani yanakuwa ya kitaifa ifikapo mwaka 2025.
Alieleza, maonyesho hayo yatasimamiwa na kuratibiwa na Wizara kwa kushirikiana na Mkoa wa Pwani, huku akisisitiza umuhimu wa kuyafanya kuwa endelevu kila mwaka.
Akifungua maonyesho ya nne ya Viwanda na Biashara Mkoa wa Pwani katika viwanja vya stendi ya zamani Mailmoja, wilayani Kibaha Disemba 15,2024 Waziri Jafo alimpongeza Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Alhaj Abubakar Kunenge, kwa kusimamia mkoa kuwa kinara wa ongezeko la viwanda na kuandaa maonyesho makubwa ya bidhaa za viwanda.
“Tunamshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuhamasisha na kuimarisha mazingira ya viwanda kwa dhamira ya kuendeleza uwekezaji nchini,” alisema Jafo.
Dkt. Jafo alieleza kuwa tangu Rais Samia aingie madarakani, idadi ya viwanda imeongezeka kutoka 52,000 mwaka 2021 hadi kufikia 80,000 mwaka 2024, ongezeko la viwanda 18,000 ndani ya miaka minne.
Aidha, katika kipindi hicho, viwanda 131 vimejengwa mkoani Pwani, hatua iliyoufanya mkoa huo kuwa kinara wa ujenzi wa viwanda nchini.
“Maeneo ya uwekezaji wa viwanda (industrial parks) yalikuwa 20 mwaka 2021, lakini sasa yamefikia 27, Kwa upande wa ajira, idadi ya wanafunzi wanaohitimu vyuo vikuu iliongezeka kutoka 51,000 mwaka 2021 hadi 67,000 mwaka 2024,” alifafanua.
Dkt.Jafo aliongeza, si wote wanaohitimu vyuo vikuu wana nafasi za kuajiriwa moja kwa moja, hivyo viwanda vinaendelea kuwa sehemu muhimu ya kuwapatia ajira vijana.
“Tuna kila sababu ya kujivunia ongezeko hili la viwanda kwa kuwa linatoa fursa za ajira ,kipato kwa vijana wetu na kuinua pato la Taifa,” alisisitiza Dkt Jafo.
Pia, alitaja changamoto ya umeme wa uhakika katika baadhi ya maeneo ya wawekezaji, akisema kuwa Serikali inaendelea kushughulikia changamoto hiyo kupitia miradi mikubwa, kama bwawa la Mwalimu Nyerere linalotarajiwa kutoa megawati 2,115 za umeme baada ya kukamilika.
Dkt. jafo aliwataka wawekezaji, kuchangamkia fursa za soko huru la kikanda na kimataifa, ikiwemo China na Jumuiya ya SADC.
Awali, Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Alhaj Abubakar Kunenge, alieleza kuwa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) linaendelea usambazaji bomba la gesi kutoka Ubungo, huku usambazaji wa gesi hiyo ukitegemewa kufanyika kupitia magari .
Aliomba wapelekewe Bomba Mkoani kwani kuna fursa ya wingi wa viwanda.
Kunenge alieleza mwaka 2023, Mkoa wa Pwani ulikuwa na umeme wa megawati 118, lakini sasa umeongezeka kwa megawati 140, ongezeko la asilimia 19, hatua iliyopunguza kero ya kukatika kwa umeme viwandani.
“Mkoa wa Pwani ni eneo sahihi la uwekezaji, na tumeendelea kutenga maeneo ya kutosha kwa ajili ya viwanda,” alisema Kunenge.
Aliongeza kuwa kutokana na mazingira bora ya uwekezaji na juhudi za taasisi wezeshi katika kuboresha miundombinu, mkoa unatarajia kuongeza idadi ya viwanda kwa asilimia 30.
Kwa mujibu wa Kunenge, Mkoa wa Pwani una jumla ya viwanda 1,533, ambapo vikubwa ni 124 na vya kati ni 120,ambapo Rais Samia aingie madarakani, viwanda vipya 78 vimejengwa, sawa na ongezeko la asilimia 63.