*Migogoro kati ya wananchi na Hifadhi sasa basi
Na Mwandishi wetu, Rukwa
Hatua iliyochukuliwa na Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania – TAWA ya kuruhusu shughuli za uvuvi endelevu ambazo awali hazikuwa zinafanyika ndani ya Pori la Akiba Uwanda lililopo wilaya ya Sumbawanga Mkoani Rukwa imekuwa chanzo cha kupungua Kwa ujangili, ongezeko la samaki Ziwa Rukwa na mapato Serikalini.
Kauli hiyo imetolewa na Kamanda wa Pori la Akiba Uwanda Nicola Thomas Desemba 17, 2024 akiongea na waandishi wa vyombo mbalimbali vya habari wakati wa ziara ya kukagua shughuli za uvuvi ndani ya hifadhi hiyo.
“TAWA kupitia Pori la Akiba Uwanda ilibuni chanzo kipya cha mapato ambacho ni kuruhusu uvuvi endelevu kuweza kufanyika ndani ya Hifadhi lengo likiwa ni kuondoa migogoro iliyokuwepo kabla kati ya hifadhi na wananchi lakini pia kuongeza mapato Serikalini kupitia shughuli hizo” amesema Kamanda Nicola
“Kipindi cha nyuma Pori la Akiba Uwanda lilikuwa halizalishi mapato yoyote Serikalini lakini tokea tulipoanza mwaka 2021, tulianza na mapato ya TZS Millioni 691 lakini mpaka mwaka 2023/24 tuliweza kuingiza mapato zaidi ya TZS Billioni moja ” ameongeza Nicola.
Kamanda Nicola amesema utaratibu wa kuanzisha forodha maalumu na kudhibiti ujangili umeinufaisha Halmashauri ya Sumbawanga na kufanya mapato yake kuongezeka mara dufu.
Aidha amesema TAWA itaendelea kuimarisha uhifadhi na ulinzi wa rasilimali zilizopo ndani ya hifadhi hiyo ikiwemo kuhakikisha wavuvi wanavua Kwa taratibu zilizowekwa na dhana zinazoruhusiwa na Wizara ya Uvuvi ili kuongeza mapato zaidi Serikalini.
Wananchi wa Mkoa wa Rukwa wameipongeza Serikali kupitia TAWA Kwa hatua hiyo ya kuruhusu shughuli za uvuvi ndani ya hifadhi ya Uwanda jambo ambalo wanakiri limewafanya waachane na ujangili, wafanye shughuli za uvuvi kwa uhuru na kupata samaki Kwa wingi sambamba na kuongeza kipato tofauti na awali ambapo walikuwa wakifanya kazi hizo Kwa kujifichaficha hali iliyopelekea kushindwa kupata kipato cha kuwatosheleza.
“Tangu TAWA imetoa ruhusa ya sisi kuvua samaki Kwa vibali maalumu, tunanufaika sana, tunavua (samaki) vizuri, tunapata samaki wengi na wazuri na hatusumbuliwi na wahifadhi wanatulea vizuri” amesema Albano Aloyce Kisanga mvuvi wa forodha ya Nangori
Kwa upande wake Afisa Habari wa TAWA Beatus Maganja amesema Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii imekuwa ikihimiza Taasisi zote zilizo chini ya wizara kubuni vyanzo mbalimbali vya mapato ili kuongeza mapato Serikalini jambo ambalo TAWA imeendelea kutekeleza katika maeneo mbalimbali hususani hifadhi ya uwanda ambayo ilikuwa haizalishi chochote
Aidha Maganja amesema licha ya kuongeza mapato TAWA imefanikiwa kuondoa migongano baina ya wananchi na hifadhi na kusisitiza kuwa imeandaa mikakati thabiti ya kuongeza mapato zaidi kwa kuongeza vitendea Kazi ikiwemo boti za doria ili kudhibiti ujangili na upotevu wa mapato.