Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), Mhe.Jaji (Rufaa) Jacobs Mwambegele, akizungumza wakati akifungua mkutano wa siku moja wa Tume na Wadau wa Uchaguzi uliofanyika leo Desemba 15, 2024 mkoani Mbeya ikiwa ni maandalizi ya Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura ambao unataraji kuanza Disemba 27 hadi Januari 02,2024. Wadau hao ni pamoja na Viongozi wa vyama vya siasa, Viongozi wa Dini, Wawakilishi wa Asasi za Kiraia, Wahariri wa Vyombo vya habari, Waandishi wa habari, Maafisa Habari wa Mikoa na Halmashauri, Wawakilishi wa Makundi mbalimbali ya Vijana, Watu wenye ulemavu, Wanawake na Wazee wa Kimila.
Na Waandishi wetu Mbeya
Mwenyekiti wa Tume Huru ya
Taifa ya Uchaguzi Jaji wa Mahakama ya Rufaa Mhe.Jacobs Mwambegele amesema kuwa
uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura katika Mikoa ya Iringa, Mbeya na
Dodoma katika Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa umepangwa kuanza tarehe 27
Disemba mwaka huu.
Akifungua Mkutano wa wadau wa
uchaguzi katika ukumbi wa Benki Kuu leo jijini Mbeya, ikiwa ni maandalizi ya
kuanza kwa uboreshaji wa Daftari katika mikoa hiyo Mhe. Jaji Mwambegele amesema
kuwa zoezi hilo litafanyika kwa muda wa siku saba kuanzia tarehe 27 Desemba,
2024 na kukamilika tarehe 02 Januari, 2025 na ambapo vituo vitakuwa
vinafunguliwa kuanzia saa 2:00 asubuhi na kufungwa saa 12:00 jioni.
Ameongeza kuwa pindi zoezi la
uboreshaji wa Daftari katika mikoa ya Iringa na Mbeya litakapokamilika, Tume
itakuwa imekamilisha mzunguko wa nane kati ya mizunguko 13 ya uboreshaji wa
Daftari.
Aidha, Jaji Mwambegele
ameeleza kuwa tangu uzinduzi wa uboreshaji wa Daftari kufanyika mnamo tarehe 20
Julai, 2024, Tume imekwishakamilisha uboreshaji wa Daftari katika Mikoa 21
nchini.
Mhe. Jaji Mwambegele ameitaja
mikoa hiyo kuwa ni pamoja na Kigoma, Tabora, Katavi, Geita, Kagera, Mwanza,
Shinyanga, Mara, Simiyu, Manyara, Dodoma na Singida. Mikoa mingine, ni pamoja
na Mikoa ya Mjini Magharibi, Kusini Unguja, Kaskazini Unguja, Kusini Pemba na
Kaskazini Pemba iliyopo Zanzibar.
Jaji Mwambegele ameongeza kuwa
hivi sasa uboreshaji wa Daftari unafanyika katika mikoa miwili ya Arusha na
Kilimanjaro na Tume inatarajia kukamilisha zoezi hilo katika mikoa hiyo mnamo
tarehe 17 Desemba, 2024.
Akifungua Mkutano wa Wadau wa
Uchaguzi katika Mkoa wa Iringa, Makamu Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya
Uchaguzi Mhe. Jaji wa Rufaa (Mst) Mbarouk Salim Mbarouk amewataka wadau wa
uchaguzi kuwahamasisha wananchi wenye sifa za kuandikishwa au wanaotarajia
kuhamisha au kuboresha taarifa kwenye maeneo husika watumia fursa hii.
Ameongeza kuwa kufanikiwa kwa
uboreshaji wa Daftari, kunategemea sana ushiriki wa wadau wa uchaguzi katika
kutoa elimu na kuhamasisha wananchi wenye sifa za kuandikishwa au wanaotarajia
kuhamisha au kuboresha taarifa zao.
“Hivyo, ni matarajio ya Tume
kuwa mtakuwa mabalozi wazuri wa kusambaza taarifa na kuwahamasisha wananchi
kujitokeza kwa wingi kujiandikisha na kuboresha taarifa zao ili zoezi hili
lifanyike kwa ufanisi na kwa mafanikio makubwa,” ameeleza Jaji Mbarouk.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa
Uchaguzi Bw. Kailima Ramadhani katika mada yake kwa wadau wa uchaguzi mkoani
Mbeya amesema kuwa kwa Mkoa wa Mbeya jumla ya vituo vya kuandikisha wapiga
kura 1,577 vitatumika kwenye uboreshaji wa Daftari kwa
mwaka huu ikiwa ni ongezeko la vituo
66 katika vituo 1,511 vilivyotumika kwenye uboreshaji
mwaka 2019/20.
Mkoani Iringa kuna vituo
1,367 vitakavyotumika kwenye uboreshaji
kwa mwaka huu ikiwa ni ongezeko la vituo 140 katika vituo 1,227 vilivyotumika kwenye uboreshaji mwaka
2019/20.
Mikutano hiyo ambayo lengo
lake ni kupeana taarifa kuhusu hatua mbalimbali zilizochukuliwa na
zinazoendelea kuchukuliwa na Tume ili kufanikisha zoezi la uboreshaji wa
Daftari imehudhuriwa na Wajumbe wa Tume, Mhe. Asina Omari ambaye alishiriki
mkutano huo mkoani Iringa na Mhe. Dkt. Zakia Mohamed Abubakar ambaye alishiriki
mkutano wa wadau mkoani Mbeya.
Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) Bw. Kailima Ramadhani akitolea majibu hoja mbalimbali za wadau wa uchaguzi.
Wadau wa uchaguzi kutoka Mkoa wa Mbeya wakiwa katika mkutano huo.
Wadau wa uchaguzi kutoka Mkoa wa Mbeya wakiwa katika mkutano huo.
Wadau wa uchaguzi kutoka Mkoa wa Mbeya wakiwa katika mkutano huo.
Mjumbe wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Mhe. Dkt. Zakia Mohamed Abubakar akizungumza wakati wa kufunga kikao hicho.