Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Harrison Mwakyembe (kulia) akisalimiana na Mkuu wa Mkoa wa Tanga Martine Shigela (kushoto) mara baada ya kuwasili mkoani humo kwa ziara ya siku mbili (Januari 7-8, 2020) kujionea namna Shirika la Utangazaji la Taifa (TBC) linavyoboresha usikivu wa matangazo yake ili wananachi wa mkoa wa Tanga waendelee wapate haki yao ya msingi ya kupata taarifa kupitia shirika hilo.
Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Anna Mghwira akiongea na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Harrison Mwakyembe (hayupo pichani) alipowasili mkoani humo kwa ziara ya siku mbili (Januari 9-10, 2020) kujionea namna Shirika la Utangazaji la Taifa (TBC) linavyoboresha usikivu wa matangazo yake ili wananachi wa mkoa wa Kilimanjaro waendelee wapate haki yao ya msingi ya kupata taarifa kupitia shirika hilo.
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Harrison Mwakyembe (wa tatu kulia) akiwa katika picha ya pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mrisho Gambo (wa nne kushoto) alipowasili mkoani humo kwa ziara ya siku mbili (Januari 11-12, 2020) kujionea namna Shirika la Utangazaji la Taifa (TBC) linavyoboresha usikivu wa matangazo yake ili wananachi wa mkoa wa Arusha waendelee wapate haki yao ya msingi ya kupata taarifa kupitia shirika hilo.
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Harrison Mwakyembe (wa kwanza kulia) akiangalia mitambo ya Shirika la Utangazaji la Taifa (TBC) ya kurushia matangazo iliyopo eneo la Kwemashai wilaya ya Lushoto mkoani Tanga alipokuwa ziara ya kikazi (Januari 8, 2020) kujionea namna shirika hilo linavyoboresha usikivu wa matangazo yake ili wananachi wa mkoa wa Tanga waendelee kupata haki yao ya Kikatiba ya kupata taarifa kupitia shirika hilo. Wa pili kulia ni Mkuu wa wilaya ya Lushoto Januari Lugangika.
……………….
Na Eleuteri Mangi-WHUSM, Arusha
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Harrison Mwakyembe amesema Shirika la Utangazaji la Taifa (TBC) ni chombo muhimu kwa wananchi kuweza kupopata taarifa na kujua matukio mbalimbali yanayotokea nchini kwa mustakabali wa taifa ili wananchi waweze kujiletea maendeleo.
Waziri Dkt. Mwakyebe amesema hayo alipokuwa akihitimisha ziara yake ya Kanda ya Kaskazini ambapo alitembelea mikoa ya Tanga, Kilimanjaro na Arusha kwa lengo la kuangalia hali ya usikivu wa Redio ya Taifa TBC inayowarahisishia wananchi katika mikoa hiyo kupokea taarifa za maendeleo ya nchi yao.
“Suala la wananchi kupata taarifa sahihi na kwa wakati sio la hiyari, ni suala la Kikatiba, tunatekeleza hitaji la Katiba Ibara ya 18 (d) ‘Kila mwananchi anahaki ya kupata taarifa ya masuala mbalimbali yanayomhusu yanayohusu maendeleo ya taifa na ni wajibu wa Serikali ya awamu ya tano kufanya hivyo’” alisema Dkt. Mwakyembe.
Aliendelea kusema “Namshukuru sana Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwamba aliliona hili mapema ameingia tu madarakani wakati usikivu wa TBC Taifa ambayo ni redio yetu ulikuwa ni 54 tu nchi nzima, sasa hivi tunaongea ni asilimia 73 na tunatarajia ifikapo mwishoni mwa mwaka 2020 usikivu utafikia zaidi ya asilimia 90 nchi nzima” Dkt. Mwakyembe.
Akiwa mkoani Tanga alitembelea kituo cha mitambo ya kurushia matangazo kiliyopo Mnyusi Hale wilayani Korogwe ambapo TBC Taifa inarusha matangazo katika masafa ya FM 87.7 Mhz na TBC FM inarusha matangazo katika masafa ya FM 89.7 Mhz wakati wilayani Lushoto mitambo ya TBC Taifa ipo katika eneo la Kwemashai wilaya ya Lushoto inarusha matangazo yake katika masafa ya FM 87.9 Mhz na TBC FM inarusha matangazo katika masafa ya FM 89.9 Mhz.
Katika mkoa wa Kilimanjaro Waziri Dkt. Mwakyembe alitembelea kituo cha TBC Taifa cha Mabungo kilichopo wilaya ya Moshi kinarusha matangazo katika masafa ya FM 87.9 Mhz na TBC FM katika masafa ya FM 90.0Mhz wakati Kituo cha Tarakea kilichopo wilayani Rombo, TBC Taifa inarusha matangazo yake katika masafa ya 87.9 Mhz na TBC FM inarusha katika 90.0Mhz.
Aidha, Dkt. Mwakembe katika mkoa wa Arusha alitembelea mitambo ya TBC Taifa iliyopo eneo la Themi katika Jiji la Arusha ambapo matangazo yake yanapatikana katika masafa ya FM 87.7 Mhz na TBC FM inayorusha matangazo katika masafa ya FM 89.9 Mhz na kuhitimisha ziara yake kwa kutembelea kituo cha TBC cha Namanga kilichopo katika wilaya ya Longido.
Katika ziara hiyo, Waziri Dkt. Mwakyembe amepata taarifa katika mikoa hiyo ambapo zipo changamoto mbalimbali ilipo mitambo ya TBC ikiwa ni pamoja na ubovu wa barabara ambao unapelekea ugumu wa kufikika kwa urahisi maeneo hayo.
Maeneo ambayo barabara ni mbovu na zinahitaji kujengwa kwa kiwango cha lami ama kujengwa kwa zege ni pamoja na Mnyusi kilichopo Hale wilaya ya Korogwe na Kwemashai wilaya ya Lushoto mkoani Tanga; Mabungo kilichopo wilaya ya Moshi mkoani Kilimanjaro pamoja na kituo cha Namanga kilichopo katika wilaya ya Longido mkoani Arusha.
Aidha, maeneo hayo pia yanahitaji kuwepo kwa miundombinu ya umeme wa uhakika ili kuhakikisha radio inakuwa hewani wakati wote na wananchi waendelee kupata haki yao ya Kikatiba ya kupata taarifa sahihi na kwa wakati za shughuli mbalimbali za Serikali kwa manufaa yao na taifa kwa ujumla.
Nao kwa upande wao Wakuu wa mikoa hiyo Martine Shigela (Tanga), Anna Mghwira (Kilimanjaro) pamoja na Mrisho Gambo (Arusha) wamemhakikishia Waziri Dkt. Mwakyembe suala la miundombinu ya barabara pamoja na umeme katika maeneo ilipo mitambo ya TBC, kwao ni kipaumbele ili redio ya Taifa iweze kusikika katika maeneo yao na wananchi wapate taarifa zitakazowasaidia katika shughuli za kila siku ikiwemo kilimo, ufugaji, uvuvi pamoja na taarifa za utalii ikizingatiwa Kanda ya Kaskazini uchumi wake unachangiwa na sekta ya utalii .
Kwa mujibu wa Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt. Hamis Kigwangalla katika Hotuba yake ya Bajeti Wizara hiyo kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 alisema kuwa idadi ya watalii walioingia nchini imeongezeka kutoka 1,327,143 mwaka 2017 hadi kufikia watalii 1,505,702 mwaka 2018. Ongezeko hilo limechangia kuongezeka kwa mapato yatokanayo na utalii kutoka Dola za Marekani bilioni 2.2 mwaka 2017 hadi kufika Dola za Marekani bilioni 2.4 mwaka 2018.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Ufundi wa Shirika la Utangazaji la Taifa (TBC) Mhandisi Upendo Mbelle aliyeambatana na Waziri Dkt. Mwakyembe kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa shirika hilo Dkt. Ayub Rioba amesema kuwa ziara hiyo imekuwa na mafanikio makubwa kwa shirika hilo na kuahidi vitu vyote vilivyo ndani ya uwezo wa TBC wamevichukua na watavifanyia kazi.
Mhandisi Upendo ameongeza kwa vitu ambavyo vipo kisera amemuoba Waziri Serikali ivipatie ufumbuzi hatua itakayosaidia shsirika kufikia malengo yake ikiwemo miundombinu ya umeme na barabara ili kuhakikisha usambazaji wa matangazo ya Redio ya Taifa yanawafikia wananchi wote katika maeneo yao ili kuwa na tija kwa shirika na taifa kwa ujumla wakiamini kwao mradi namba moja ni usikivu wa redio hiyo kwa wananchi.
TBC ni shirika la utangazaji la umma lililoanzishwa kwa mujibu wa Sharia ya Mashariki ya Umma ya mwaka 1992 kutoa huduma ya utangazaji kwa umma kwa njia ya redio na televisheni na kupewa mamlaka ya kutangaza vipindi mbalimbali vinavyoakisi misingi ya maadili ya Kitanzania kupitia vipindi vya elimu na burudani; kutoa habari za aina mbalimbali, taarifa na uchambuzi kwa mtazamo wa Kitanzania na kuendeleza maslahi ya taifa na ya umma.