Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Peter Lijualikali wakati akizungumza Kwenye warsha ya kupinga mimba na ndoa za utotoni
Baadhi ya wadau walioshirika katika warsha ya kufunga mradi wa kupinga mimba na ndoa za utotoni.
Picha na Neema Mtuka
Mkurugenzi wa shirika la Plan International Laurence Wambura wakati akimkabidhi mgeni rasmi nyenzo za uendelevu wa shughuli za mradi wa kupinga mimba na ndoa za utotoni kwa Halmashauri.
Sekretarieti ya mkoa katika picha ya pamoja na wadau wa kupinga mimba na ndoa za utotoni.
……………………
NEEMA MTUKA – SUMBAWANGA
Rukwa: Jamii mkoani Rukwa imetakiwa kuachana na mila na desturi zinazomkandamiza mtoto wa kike ili kupunguza kasi ya ongezeko la mimba na ndoa za utotoni.
Hayo yamesemwa na Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga, Peter Lijualikali, wakati akimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Charles Makongoro Nyerere, kwenye warsha ya kufunga mradi wa kupinga mimba na ndoa za utotoni, iliyofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Mkoa wa Rukwa.
Amesema lengo la warsha hiyo ni kuielimisha jamii juu ya athari za mimba na ndoa za utotoni, huku akisisitiza kuwa sheria mbalimbali zimewekwa ili kupambana na changamoto hiyo.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Miradi wa shirika la Plan International, Laurance Wambura, utafiti wa Demografia na Viashiria vya Malaria wa mwaka 2022 unaonyesha kuwa asilimia 29.6 ya wanawake wenye umri wa miaka 15-19 mkoani Rukwa tayari ni wajawazito au wamezaa, kiwango kinachozidi wastani wa kitaifa wa asilimia 22.
Tangu kuanzishwa kwa mradi wa kupinga mimba na ndoa za utotoni mwaka 2020, kumekuwa na mafanikio makubwa. Mfano, matukio 269 ya ndoa za utotoni yaliripotiwa kwa kamati za ulinzi wa mtoto mkoani Rukwa, yakiwa yamesambazwa kama ifuatavyo: Nkasi (115), Kalambo (54), Sumbawanga Vijijini (83), na Manispaa ya Sumbawanga (17).
Baadhi ya wanafunzi walioshiriki warsha hiyo, akiwemo Nestory Wangao na Jane Rose Ismail wa Shule ya Sekondari Mazwi, walisema mradi huo umewapa nguvu ya kupambana na mimba na ndoa za utotoni.
“Mradi wa Plan International umeleta mabadiliko makubwa. Wasichana waliopata mimba wamenufaika na vitendea kazi kama cherehani, ambavyo vinawasaidia kujipatia kipato na kuwaelimisha wengine,” alisema Jane.
Sheikh wa Mkoa wa Rukwa, Rashid Akilimali, aliwahimiza wazazi na walezi kuwasomesha watoto wa kike na kuacha tabia ya kuwaona kama kitega uchumi. Askofu wa KKKT Dayosisi ya Ziwa Tanganyika, Imani Chibona, alionya juu ya mmomonyoko wa maadili, akisema:
“Hali ni mbaya; wazazi wengi hawana muda wa kuzungumza na watoto wao. Malezi bora ni silaha muhimu ya kukabiliana na changamoto hizi.”
Kwa upande wa Jeshi la Polisi, Mkuu wa Dawati la Jinsia na Watoto, Faustina Mwagala, alibainisha kuwa mila kandamizi bado ni changamoto kubwa. Alipendekeza marekebisho ya sheria ya mwaka 2009 ili kuimarisha ulinzi wa mtoto wa kike.
Naye Afisa Elimu wa Sekondari Wilaya ya Kalambo, Ramadhani Mabula, alieleza kuwa ushirikiano kati ya wazazi, viongozi wa dini, walimu, na serikali umepunguza matukio ya mimba na ndoa za utotoni. Shule zimeanzisha vilabu vinavyowasaidia wanafunzi kujadili mbinu za kukabiliana na changamoto hizi.
Kwa upande wake, Mwakilishi wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Watoto, na Makundi Maalum, Job Kapala, alielezea lengo la Mpango wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto (MTAKUWA), kuwa ni kuimarisha malezi na kuleta mazingira salama kwa watoto na wanawake.
Warsha hiyo, iliyoshirikisha mashirika mbalimbali kama Plan International, RUSUDEO, YES Tanzania, na Dawati la Jinsia na Watoto, ilihitimishwa kwa mipango ya mkakati wa mradi ujao.