………………..
Na Sixmund Begashe – Mikumi.
Serikali kupitia Mradi wa Kuboresha Usimamizi wa Maliasili na Kukuza Utalii Kusini mwa Tanzania (REGROW) imeweza kubadili maisha ya wakazi wa Kijiji cha Mikumi kutokana na shughuli mbalimbali wanazozifanya kwenye vikundi vya Kijamii pamoja na jitihada za mtu moja moja.
Akizungumza na waandishi wa habari waliopo kwenye ziara ya kutembelea Mradi huo, Afisa Mtendaji Kata ya Mikumi Bw. Ramadhan Msaga amesema, uwepo wa vijiji hivyo jirani na Hifadhi ya Taifa Mikumi imekuwa neema kwa wananchi kwa kuwa utekelezaji wa mradi wa REGROW, umeweza kuwapatia zaidi ya Milioni 600 wanachama 327 waliopo kwenye vikundi 15 ili zitumike kuinua shughuli za kujipatia kipato kwa mfumo wa Benki za Jamii (COCOBA).
Bw. Msaga amesema kuwa, ni fahari kubwa kwa Serikali ya Kijiji cha Mikumi kuona watu wake hususani Wanawake na Vijana wanakua kiuchumi kwani licha ya kuongeza hali ya amani na utulivu miongoni mwa jamii pia inaimarisha usalama wa maeneo yaliyohifadhiwa kisheria wakiwemo wanyamapori na ikolojia ya Hifadhi ya Taifa Mikumi.
Naye Katibu wa Kikundi cha Tumaini Tambukareli COCOBA, kinachojishughulisha na ufugaji wa Nguruwe, Bi. Pendo Mosha amesema, hadi sasa wananguruwe wanne wenye mimba ambao muda si mrefu watazaa na kupata watoto zaidi ya 50 ambao wanatarajia kupata faida ya zaidi ya Tsh 15, 000,000/=
Aidha, Katibu wa Kikundi cha Masai Boma Bw. Nuhu Meleni amesema kupitia Mradi wa REGROW licha ya mafanikio ya kikundi yeye mwenyewe binafsi ameweza kunufaika kwa kujenga nyumba ya kisasa, kulea familia yake, kusaidia ndugu na jamaa wengine.
Akizungumzia manufaa ya mradi wa REGROW kwa wanamikumi Bi. Neema Mgalambe (Mwezeshaji Jamii), ameseme licha ya neema kubwa kwa wananchi kupitia COCOBA, pia mradi wa REGROW umetoa ufadhili wa masomo kwa vijana 87 wanawake 52 wanaume 35 katika fani tofauti tofauti ikiwemo uhifadhi, utalii, upishi, udereva , ufundi mitambo huku vijana wengi wao wamehitimu na kati yao, kumi 10 wamepata ajira za kudumu na ajira za muda, wanawake 6 na wanaume 4 huku ufadhili wa Masomo hayo ukigharimu zaizi ya Milioni 500