Happy Lazaro, Arusha .
Naibu Waziri wa fedha,Hamad Hassan Chande amewataka Wahitimu katika Chuo cha uhasibu Arusha kutumia tafiti zao kuisaidia jamii kukabiliana na changamoto kwenye maeneo waliyoyabaini na kuyafanyia tafiti.
Ameyasema hayo leo mkoani Arusha kwa niaba ya Waziri wa fedha ,Dkt.Mwigulu Nchemba kwenye mahafali ya 26 ya wahitimu wa Chuo cha uhasibu Arusha ambapo jumla ya wahitimu 5854 wametunikiwa astashahada, stashahada,shahada na shahada za uza
Amesema kuwa,endapo watabaki na matokeo ya tafiti hizo watakuwa hawajawasaidia watanzania,kwani itakuwa vema kama wale walioshirikishwa kwenye tafiti zao watapata mrejesho wa kile kilichokuwa kikifanyiwa utafiti ili waweze kufanyia kazi .
“Tafiti zenu zisiishie kwenye maktaba au machapisho baada ya kuhitimu,shirikisheni jamii matokeo ya tafiti zenu yatumike kama.chachu katika kuleta mabadiliko chanya,kuongeza tija kwenye shughuli za kiuchumi na kijamii ,utendaji kazi wa kila siku katika taasisi mbalimbali za umma na binafsi ,usimamizi wa taasisi na mashirika, uboreshaji wa sera,mipango na mikakati kwa ustawi wa taasisi, mashirika ,jamii na maslahi mapana ya Taifa.”amesema Chande.
Aidha amesema kuwa, kadri watakavyokuwa waadilifu ,wabunifu,wazalendo na watakapojituma katika kazi watakazoenda kuzifanya katika maeneo mbalimbali kwenye sekta ya umma na binafsi ndivyo watakavyoionesha thamani na tija ya elimu waliyoipata Chuo cha uhasibu Arusha.
Kwa upande wake Mkuu wa chuo hicho,Profesa Eliamani Sedoyeka amesema kuwa ,chuo hicho kimeendelea kutekeleza majukumu yake ya msingi ya kutoa mafunzo,kufanya tafiti na kutoa ushauri wa kitaalamu unaoendana na taaluma zinazotolewa chuoni,kuanzia ngazi ya Astashahada,Stashahada,Shahada na Shahada ya Uzamili.
Aidha amewataka wahitimu hao kwenda kudhibitisha umahiri na weledi wao popote watakapotumikia umma katika maeneo ya usalama wa mtandao, utalii,ukutubi na usimamizi wa elimu.
Profesa Sedoyeka amesema kuwa,Chuo kimeendelea kuimarisha ushirikiano na taasisi nyingine za serikali ikiwa ni pamoja na majeshi yetu hapa nchini ikiwemo jeshi la wananchi wa Tanzania ,jeshi la Magereza na Jeshi la Polisi.
Amefafanua kuwa,katika mwaka wa masomo 2023/2024 chuo hicho kilianzisha ushirikiano na jeshi la polisi kupitia shule ya polisi Tanzania katika utoaji wa mafunzo katika maeneo mbalimbali.
“Mwaka huu mwezi Septemba pia tumeingia makubaliano na jeshi la magereza kupitia chuo cha Urekebishaji katika kutoa mafunzo kwenye maeneo mbalimbali na tunaahidi kuendeleza ushirikiano na wadau mbalimbali wa elimu ndani na nje ya nchi kama sehemu ya kuboresha zaidi ujifunzaji na ufundishaji ili kuhakikisha tunatimiza kikamilifu majukumu yetu kama Taasisi ya elimu ya juu kusaidia jamii na Taifa letu.”amesema.
Amefafanua kuwa ,dhamira ya chuo ni kuendelea kuanzisha mitaala inayokidhi mahitaji ya soko la ajira kwa wahitimu wao .na kuwawezesha kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya sayansi na teknolojia.
“Katika mwaka wa masomo wa 2025/2026 tunatarajia kuanzisha mitaala mipya minne, miwili ikiwa ni ya shahada ya kwanza na miwili ya Stashahada ambapo kupitia mradi wa elimu ya juu kwa mageuzi ya kiuchumi katika mwaka wa masomo 2025/2026 tunatarajia kuhuisha mitaala 18 ili kuendana na mahitaji ya soko la ajira,kujumuisha masuala ya elimu jumuishi na jinsia pamoja na masuala ya mabadiliko ya tabia nchi.
Profesa Sedoyeka amesema kuwa,misingi ya chuo hicho ni umahiri na weledi na kwamba katika kuiishi misingi hii chuo kitaendelea kuanzisha kozi za kimkakati zinazoendana na mahitaji ya soko letu la sasa hapa nchini.
Naye Mwenyekiti wa baraza la uongozi wa Chuo cha Uhasibu Arusha,Dkt.Mwamini Tulli amesema kuwa,kazi yao kama baraza la uongozi wa.chuo ni kuhakikisha wanaendelea kushirikiana nao ili malengo,mipango na mikakati waliyojiwekea inatekelezwa na chuo kinabaki katika hadhi ya heshima ambayo imejengwa kw muda mrefu inalindwa kwa nguvu zote.
Ameongeza kuwa,moja ya malengo katika mpango mkakati wa chuo 2021/2022-2025/2026 ni kuongeza idadi ya wanafunzi kila mwaka wa masomo ili tuweze kufikisha huduma ya elimu kwa watanzania wengi na wasio watanzania na ili kutimiza lengo hilo chuo kimeendelea kufanya uwekezaji katika ukarabati wa miundombinu iliyopo na kujenga miundombinu mingine ili kupata uwezo wa kuchukua wanafunzi wengi kwa wakati mmoja.