Na Mwandishi Wetu – Kinondoni
Aliyekuwa Mhasibu wa Klabu ya Mpira wa Miguu ya Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni (KMC FC), Bw. Atulinda Barongo, amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kivukoni, Kinondoni, Dar es Salaam, akikabiliwa na tuhuma za uhujumu uchumi.
Bw. Barongo anashtakiwa kwa ubadhirifu wa fedha kiasi cha shilingi milioni 8.91, kinyume na kifungu cha 28(1) cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, Sura ya 329 kama ilivyorekebishwa mwaka 2019.
Aidha, anatuhumiwa kutumia nyaraka za kughushi kwa lengo la kumdanganya mwajiri wake, kinyume na kifungu cha 22 cha sheria hiyo hiyo.
Mashtaka hayo yalisomwa na Wakili wa TAKUKURU, Aidan Samali, mbele ya Hakimu Josiah, ambapo Bw. Barongo alikanusha mashtaka yote.
Kesi hiyo imepangwa kusikilizwa hoja za awali tarehe 19 Desemba 2024.