Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Mahmoud Thabit Kombo (Mb.) amewatunuku vyeti wahitimu 893 wa masomo katika Kituo cha Uhusiano wa Kimataifa cha Dkt. Salim Ahmed Salim na kuwausia mambo muhimu yatakayowasaidia katika maisha baada ya kuhitimu.
Akihutubia wakati wa Mahafali hayo ya 27, Waziri Kombo amewaeleza wahitimu yakuwa yapo mambo ambayo endapo watayafuata wataweza kufanikiwa katika sekta yoyote watakayobahatika kufanya kazi ikiwemo; kuwa na dhamira thabiti ‘determination’ katika utekelezaji wa majukumu wanayopaswa, kuwa na shauku ama mapenzi ‘passion’ na majukumu yao pamoja na kujidhatiti katika utekelezaji wa majukumu ili kuyakamilisha kwa ufanisi na weledi.
Waziri Kombo amewataka pia kuwa majasiri katika kujielezea kwani wana nafasi nzuri ya kuwa mabalozi wazuri wa Tanzania ndani na nje ya nchi. Amewataka wawe na ujuzi wa kubishana kwa hoja kwani ni moja ya mambo muhimu katika Uhusiano wa Kimataifa na Diplomasia.
“Kubishana si utovu wa nidhamu. Kubishana kwa hoja ni jambo muhimu sana,” amesema Waziri Kombo.
Ameeleza kuwa Kituo cha Uhusiano wa Kimataifa cha Dkt. Salim Ahmed Salim sasa kinashirikiana na chuo cha diplomasia kutoka Umoja wa Falme za Kiarabu kijulikanacho kama ‘Anwar Gargash Diplomatic Academy’ kwa lengo la kuanza kubadilishana wanafunzi na ujuzi katika mafunzo ya diplomasia.
Wahitimu wametakwa pia kujielimisha na kuzifahamu vyema ajenda zote za nchi ikiwemo ile ya Jenga Kesho iliyo Bora katika kilimo, Ajenda 2050 inayolenga kufikia maendeleo endelevu ya kiuchumi na kijamii na hadhi ya kipato cha juu ifikapo 2050, Ajenda ya Nishati Safi ya Kupikia na vipaumbele mbalimbali vya nchi kwa kutumia elimu waliyoipata kama sehemu ya kutatua changamoto mbalimbali za kitaifa.
Jumla ya wahitimu 893 wametunukiwa vyeti. 58 wametunukiwa Astashahada ya Awali ya Uhusiano wa Kimataifa na Diplomasia, 103 Astashahada ya Uhusiano wa Kimataifa na Diplomasia, wahitimu 120 Stashahada ya Uhusiano wa Kimataifa na Diplomasia, 229 Stashahada ya Juu ya Uhusiano wa Kimataifa na Diplomasia. Wahitimu 297 wametunukiwa Shahada ya Uhusiano wa Kimataifa na Diplomasia, wahitimu 24 wametunukiwa Stashahada ya Uzamili ya Menejimenti ya Uhusiano wa Kimataifa, 28 Shahada ya Uzamili ya Diplomasia ya Uchumi, huku wahitimu 6 na 28 wakitunukiwa Stashahada ya Uzamili ya Amani na Menejimenti ya Migogoro na Shahada ya Uzamili ya Utawwala wa Kimkakati mtawalia.