******
Na Mwandishi Wetu
Serikali ya Tanzania imesema imeweka mikakati ya kina kwa ajili ya kujenga
uwezo wa mfumo wa afya, ikiwa ni pamoja na kuidhinisha ushirikiano kati ya
sekta ya umma na binafsi.
Akizungumza Jana kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es
Salaam, Albert Chalamila katika hafla rasmi ya kufunga awamu ya kwanza ya mradi
wa kuboresha huduma za dharura za Afya Tanzania (IMECT) uliofanyika kwa
ushirikiano wa taasisi za umma na binafsi unaofadhiliwa na serikali ya Poland
kupitia kituo cha msaada wa kimataifa cha Poland kwa kushirikiana na Taasisi ya
Huduma za Afya za Aga Khan Tanzania pamoja na serikali ya Tanzania Mganga Mkuu
wa Mkoa wa Dar es Salaam, Dkt. Mohamed Manguna amesema Hatua hizo zinalenga
kuhakikisha kwamba huduma za dharura zinapatikana kwa urahisi, zenye ubora, na
zinakidhi mahitaji ya wananchi kwa wakati.
Alisema Mradi huo wa IMECT wenye thamani ya TZS
Bilioni 1.8 ni mfano bora wa mafanikio ya ushirikiano, ukileta pamoja Serikali
ya Tanzania, washirika wa kimataifa, na jamii za ndani katika jitihada za
kuimarisha huduma za matibabu ya dharura kote nchini.
“Mradi wa IMECT ni mfano bora wa mafanikio ya
ushirikiano, ukileta pamoja Serikali ya Tanzania, washirika wa kimataifa, na
jamii za ndani katika jitihada za kuimarisha huduma za matibabu ya dharura kote
nchini.
Natumia fursa hii kuishukuru Serikali ya Poland
kupitia Kituo cha Msaada wa Kimataifa cha Poland (PCPM) na Huduma za Afya Aga
Khan Tanzania (AKHST) kwa hatua kubwa waliyopiga ya kutambua hitaji na kutoa
ufadhili wa kiasi cha dola za Marekani 760,000, sawa na shilingi za Kitanzania
bilioni 1.8, kwa lengo la kuboresha huduma za dharura nchini katika kipindi cha
miaka miwili na nusu iliyopita.”
Pia alipongeza huduma za Afya za Aga Khan Tanzania
kwakuwa ni mfano wa kuigwa katika ushirikiano wa sekta ya Umma na Binafsi kwa
juhudi zake za kusaidia juhudi za serikali katika kuimarisha mifumo ya afya.
Kwa upande wake Waziri wa mambo ya nje wa Jamhuri ya
Poland Jakub Wisniewski alisema wanafuraha kushirikiana na serikali ya Tanzania
kupitia Taasisi ya Huduma za afya ili kuimarisha huduma hizo za dharura
“Tunafurahi na tunajivunia kushirikiana na serikali ya
Tanzania kupitia Taasisi ya huduma za Afya za Aga Khan ili kuimarisha huduma za
dharura , kwakuwa hii ilikuwa ni mara ya kwanza Poland kuwekeza katika sekta ya
afya nchini Tanzania na kwa matokeo mazuri kama haya ni mwanzo wa uwezekano wa
ushirikiano zaidi siku zijazo”
Naye Mratibu wa Huduma za Dharura na Utunzaji Muhimu
kutoka Wizara ya Afya, Dkt. Erasto Sylvanus, aliishukuru timu za usimamizi wa
vituo vyote vilivyoshirikiana kwa uongozi na msaada wao wakati wa utekelezaji
wa mradi.
“Naipongeza Serikali ya Tanzania, kupitia
Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuunga mkono ushirikiano wa sekta
nyingi kati ya umma na binafsi ili kushughulikia mahitaji ya jamii na mifumo ya
afya.”
Dkt. Hussein K. Manji, Mratibu wa Mradi, Taasisi ya
Huduma za Afya ya Aga Khan Tanzania alisema: “Fani ya Magonjwa za Dharura
ni taaluma maalum yenyewe, na haitoshi tu kujua la kufanya, bali pia kuwa na
rasilimali na uwezo wa kutumia ujuzi huo kwa vitendo ni muhimu. Tunapojenga
uwezo na kuimarisha miundombinu, tunalenga kupunguza rufaa,kupunguza vifo, na
kuwapa wananchi wetu walioko katika hali mbaya nafasi bora zaidi ya
kupona.”