Na Ashrack Miraji, Fullshangwe Media
Tamasha kubwa la Same Utalii Festival Season 2 linatarajiwa kufanyika Desemba 20 hadi 22, 2024, Wilaya ya Same, Mkoa wa Kilimanjaro. Lengo kuu la tamasha hili ni kuunga mkono juhudi za Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kukuza na kuhamasisha sekta ya utalii nchini.
Mkuu wa Wilaya ya Same, Kasilda Mgeni, amesema maandalizi ya tamasha yanaendelea vizuri. Kabla ya siku rasmi za tamasha, kutakuwa na matukio maalum kuanzia Desemba 17 hadi 19, yakiwemo:
Utalii wa Matibabu (Tourism Clinic): Wananchi wa Same na wageni watapata matibabu bure kutoka kwa madaktari bingwa.
Safari Maalum ya Treni: Treni maalum itatoka Dar es Salaam kwenda Same Desemba 18. Treni hiyo itakuwa na mabehewa maalum yenye nyama choma, vinywaji, michezo kwa watoto, na burudani za muziki.
Desemba 20: Uzinduzi rasmi utahusisha ziara kwenye Hifadhi ya Mkomazi, ikifuatiwa na mkesha wa burudani za wasanii mbalimbali.
Desemba 21: Mbio za marathon zitafanyika, zikijumuisha kilomita 21, 10, na 5. Pia kutakuwa na ziara ya Mlima Kidenge, unaofanana na Ukuta wa China.
Desemba 22: Burudani mbalimbali zitaendelea, sambamba na maonesho ya bidhaa za wajasiriamali na mabanda maalum.
Vivutio vya utalii katika Wilaya ya Same vitakavyonogesha tamasha
Mlima Shengena: Upo ndani ya Hifadhi ya Msitu wa Chome na unavutia kwa ndege na chura wa kipekee duniani.
Hifadhi ya Mkomazi: Nyumbani kwa wanyama wa kipekee na sasa inazidi kuvutia watalii zaidi.
Tamasha la kwanza lililofanyika mwaka jana liliongeza idadi ya watalii kwenye Hifadhi ya Mkomazi kutoka 7,000 hadi 9,000 kwa mwaka. Aidha, limehamasisha ujenzi wa hoteli mpya, zikiwemo mbili zilizopo Shengena na lango la hifadhi hiyo.
Tamasha linahamasisha utalii wa ndani, kuchochea uchumi wa wananchi wa Same, na kuongeza fursa za ajira kwa wajasiriamali, wamiliki wa hoteli, na mama ntilie. Pia linasaidia katika juhudi za Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kupitia filamu The Royal Tour, inayotangaza vivutio vya Tanzania kimataifa.
“Wananchi wamehamasika sana kutokana na mafanikio ya tamasha la kwanza. Hili la mwaka huu linatarajiwa kuwa kubwa zaidi na ni fursa ya kipekee kwa Watanzania kufurahia utalii wa ndani,” alisema Mgeni.