Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Dkt. Mohamed Said Dimwa,akizungumza na Makamu Mkuu Mstaafu wa Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar (SUZA) Prof.Saleh Idrissa Mohamed na Mkewe hapo nyumbani kwake Miembeni Zanzibar katika ziara yake ya kuwatembelea wastaafu wa Serikali na Chama Cha Mapinduzi iliyofanyika leo Disemba 11,2024.
Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Dkt. Mohamed Said Dimwa, akisalimiana na Mke wa Prof.Saleh Bi.Moza Himid Mbari mara baada ya kuwasili nyumbani kwao kwa ajili ya kuwatembelea na kubadilishana mawazo.
Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Dkt. Mohamed Said Dimwa, akibadilishana mawazo na uzoefu na Makamu Mkuu mstaafu wa Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar Prof.Saleh Idrassa Mohamed mara baada ya kuwasili nyumbani kwake Miembeni Zanzibar kwa ajili ya kumtembele.
………..
Na Is-haka Omar,Zanzibar.
Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Dkt. Mohamed Said Dimwa, amesema kuwa kipaumbele cha Chama Cha Mapinduzi (CCM) ni kuisimamia Serikali iendelee kutoa huduma na kuwatumikia wananchi kwa uadilifu.
Dkt. Dimwa aliyasema hayo katika mwendelezo wa ziara yake ya kuwatembelea viongozi wastaafu wa chama na serikali pamoja na wagonjwa, alipomtembelea Makamu Mkuu mstaafu wa Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar (SUZA), Prof. Saleh Idrissa Mohamed, na mkewe Bi. Moza Himid Mbari nyumbani kwao shehia ya Miembeni, Jimbo la Kikwajuni, Unguja.
Katika ziara hiyo, Dkt. Dimwa alieleza kuwa CCM inatambua na kuthamini mchango mkubwa wa viongozi na watendaji wastaafu katika sekta za umma na binafsi, kwani maendeleo yaliyofikiwa nchini ni matokeo ya ubunifu, uchapakazi, na uzalendo wao wakati walipokuwa wakihudumu katika nafasi zao.
Akizungumzia kuhusu sera ya Serikali ya Awamu ya Nane, Dkt. Dimwa alisisitiza kuwa Serikali ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Mwinyi, imeendelea kutunza na kuwasaidia wastaafu na wazee wote bila kujali tofauti zao za kidini, kikabila, na kisiasa.
Alibainisha kuwa Serikali imeweka utaratibu wa kutoa pensheni ya shilingi 50,000 kwa mwezi kwa kila mzee ili kuwawezesha kupata huduma bora na kuishi kwa heshima.
“Chama Cha Mapinduzi kinatambua mchango wa wastaafu katika maendeleo ya nchi. Serikali ya Dkt. Mwinyi inaendelea kutekeleza sera hii ya kuwahudumia wastaafu kwa haki na usawa,” alisema Dkt. Dimwa.
Dkt. Dimwa aliwakumbusha wastaafu hao kuwa nchi bado inahitaji busara, uzoefu, na ushauri wao katika uongozi na utendaji.
Aliwaomba viongozi wastaafu kuendelea kutoa ushauri na maoni pale wanaposhuhudia upungufu katika utekelezaji wa majukumu ya Serikali, ili chama na serikali ziweze kuchukua hatua kwa wakati.
“Pamoja na mafanikio mengi, bado kuna changamoto katika utekelezaji wa majukumu. Tumekuwa tukitegemea busara yenu na uzoefu wenu ili tufikie maendeleo zaidi. Tungependa mendelee kutushauri na kutufundisha ili tusonge mbele,” alisisitiza Dkt. Dimwa.
Katika hatua nyingine, Dkt. Dimwa alitoa wito kwa wastaafu hao kuendelea kuwaombea dua viongozi wa nchi, akitaja Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, pamoja na Rais wa Zanzibar, Dkt. Hussein Mwinyi na kwamba dua hizo zitasaidia viongozi hao kuendeleza busara, hekima, na maarifa katika kuiongoza nchi kuelekea uchumi wa kisasa na maendeleo endelevu.
Pamoja na hayo, Dkt. Dimwa alitumia fursa hiyo kuzungumzia maandalizi ya CCM kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2025,alisema chama hicho kimejipanga kuhakikisha kinashinda uchaguzi kwa nguvu ya wananchi, ambao ndio wanaotoa ridhaa ya uongozi kwa chama kilichotekeleza sera za maendeleo kwa vitendo na kushughulikia changamoto zinazowakabili wananchi.
“CCM itashinda uchaguzi huu kwa nguvu ya wananchi ambao wanajua kuwa serikali yao inatekeleza haki zao za kijamii na kiuchumi. Tunaendelea na maandalizi ya kushinda kwa umoja na juhudi za pamoja endeleeni kutuunga mkono sisi tulikuja kwenu kuomba kazi, mkatatupa kazi na tunaendelea kuchapa kazi kwa kasi yenye viwango vya upekee,” alieleza Dkt. Dimwa.
B Naye Makamu Mkuu Mstaafu wa SUZA, Prof. Saleh Idrissa Mohamed, alitoa shukrani zake kwa Dkt. Dimwa kwa kuendelea kuwatembelea wastaafu na kubadilishana nao mawazo.
Alisisitiza umuhimu wa utamaduni wa kuwatembelea wazee ili kupata ushauri wa kiutendaji na uzoefu wao.
Alihimiza viongozi na watendaji wengine wa serikali kuiga mfano wa Dkt. Dimwa kwa kuendeleza mawasiliano na wastaafu ili kujenga taifa lenye ufanisi zaidi.
“Ni muhimu kwa viongozi wa sasa kuendelea kujifunza kutoka kwa wastaafu. Uzoefu wetu unaleta mafanikio na mafundisho muhimu kwa mustakabali wa taifa letu,” alisema Prof. Saleh
Ziara hii ni sehemu ya jitihada za CCM Zanzibar kuimarisha uhusiano kati ya viongozi wastaafu na viongozi wa sasa, na kuendelea kutekeleza sera za maendeleo kwa ajili ya ustawi wa wananchi wote.