Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhandisi Anthony Sanga (wa kwanza kulia) akimsililiza Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) Dkt. Sophia Kongela (katikati) wakati Wajumbe wa Bodi ya
Shirika la Nyumba la Taifa ambao wamefanya ziara kukagua ujenzi wa majengo ya wizara mbalimbali likiwemo jengo la Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi linalojengwa na shirika hilo katika Mji wa Serikali Mtumba jijini Dodoma.
Viongozi wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi na wajumbe wa Bodi ya Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) wakipata maelezo wakati wa ziara kukagua ujenzi wa majengo ya wizara mbalimbali likiwemo jengo la Wizara ya
Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi linalojengwa na shirika hilo katika Mji wa Serikali Mtumba jijini Dodoma.
……
Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhandisi Anthony Sanga ameridhishwa na ujenzi wa jengo la Wizara hiyo linalojengwa na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) katika Mji wa Serikali Mtumba jijini Dodoma.
Mhandisi Sanga amesema hayo Desemba 11, 2024 ambapo ameungana na Wajumbe wa Bodi ya Shirika la Nyumba la Taifa ambao wamefanya ziara kukagua ujenzi wa majengo ya wizara mbalimbali likiwemo jengo la Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi linalojengwa na shirika hilo katika Mji wa Serikali Mtumba.
“Leo mmejionea wenyewe maendeleo makubwa ambayo yamefanywa ambapo tumeshuhudia jengo letu limefikia takriban asilimia 90 ya ukamilishaji wa kazi zinazoendelea” amesema Mhandisi Sanga.
Aidha, Mhandisi Sanga ameelekeza Shirika la NHC kuongeza kasi ya kukamilisha ujenzi wa jengo hilo ili ifikapo Januari 2025 watumishi wa wizara hiyo waanze kulitumia na kufanya kazi katika ofisi hizo za Makao Mkao Mkuu ya Wizara.
“Kwenye ubora wa kazi hatuna mashaka nao kuanzia ‘floor’ ya kwanza hadi ya mwisho, ubora wa kazi ni mzuri na jengo lipo imara na hatuna shaka juu ya hilo, hatua inayoendelea sasa ni umaliziaji vioo vinawekwa sasa. Kwetu sisi Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Bodi inafanya kazi vizuri sana, jengo ambalo linajengwa na Shirika letu tumeridhika na ubora wake” amesema Mhandisi Sanga.
Akizungumzia ziara hiyo, Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) Dkt. Sophia Kongela amewapongeza wakandarasi wanaojenga mradi huo kwa kazi kubwa wanayofanya na kuwasisitiza kufanyakazi usiku na mchana ili kukamilisha mradi huo.
“Ndoto yetu kama Bodi tunatarajia kila mradi unaotekelezwa na shirika unapaswa kukamilika kwa wakati ili kufikia malengo ya shirika kwa kujenga majengo kulingana na mpango ulioidhinishwa” amesema Dkt. Kongela.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), Hamad Abdallah amesema shirika hilo linasimamia miradi 10 ya ujenzi wa majengo ya Wizara mbalimbali katika Mji wa Serikali Mtumba jijini Dodoma ambapo miradi nane NHC ni wakandarasi katika ujenzi likiwemo jengo la Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi na miradi miwili ni shirika hilo ni Mshauri Mwelekezi.