……..
NA NOEL RUKANUGA, DAR ES SALAAM
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Kinondoni imewajengea uwezo Wafanyakazi wa Hospitali ya Rufaa Mwananyamala kuhusu umuhimu wa kuzingatia maadili, madhara ya rushwa ya ngono pamoja na ukatili wa kijinsia katika utekelezaji wa majukumu yaoikiwemo kuepuka vitendo vya rushwa wakati wa kutoa huduma.
Akizungumza leo Disemba 11, 2024 jijini Dar es Salaam wakati akifungua warsha ya kuwajengea uwezo Wafanyakazi wa Hospitali ya Rufaa Mwananyamala ikiwa ni sehemu ya Maadhimisha siku ya maadili na haki za Binadamu, Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Mhe. Saad Mtambule, amesisitiza umuhimu watumishi wa umma kuzingatia maadili na miiko ya kazi wanapotekeleza majukumu hususani kwenye upatikanaji wa ushahidi kwenye matukio ya ukatili ikiwemo ubakaji na ulawiti.
Mhe. Mtambule amesema kuwa watumishi wa afya wanapaswa kutokuwa sehemu ya kufanikisha uhalifu na ukatili wanaofanyika katika jamii, huku akiwakumbusha kutoa ushahidi wa kweli katika kujaza fomu ya Polisi ya PF3 ili mtuhumiwa atiwe hatiani na kuwafanya wasiendelee kutekeleza matukio ya kikatili ndani ya jamii.
“Tunapaswa kuharakisha uchunguzi wa kweli na ushahidi kurudishwa Polisi ili kusaidia upatikanaji wa haki kwa wakati kwa mtenda na mtendewa, simameni kama wataalamu kwenye sekta ya Afya kwa kukataa Rushwa na kusimamia sheria za kazi ili kuendelea kulinda haki za Binadamu” amesema Mhe. Mtambule.
Amesema kuwa Wilaya ya Kinondoni bado kuna matukio ya ukatili ya ubakaji na ulawiti hususani maeneo ya Mwananyamala, Makumbusho, na Tandale, huku akitoa wito kwa viongozi wa Dini na watu wa haki Jinai kuangalia jinsi ya kukabiliana na ukatili wa kijinsia.
Mhe. Mtambule amesema Hospitali ya Rufaa ya Mwananyamala ni kimbilio ya watu wengi wazee, wazazi kutokana na unafuu wa gharama , huku akisisitiza umuhimuwa wa kutoa huduma kwa kuzingatia msingi na miiko ya utumishi wa umma ili kuwa na nguvu ya kuzungumzia rushwa na kuepuka uzembe na maadili mabovu.
“Nisisitiza kuishi na kutenda kazi kwa kuzingatia miiko ya utumishi wa umma ambayo ni uadilifu, uzalendo, utaratibu wa kuwasiliana, kuongea matumizi ya lugha nzuri kwa wagonjwa, mavazi kulingana na miiko ya kazi” Mhe. Mtambule.
Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Kinondoni Bw. Christian Nyakizee amesema lengo la warsha ni kuwakumbusha watumishi wa umma kutekeleza majukumu yao bila kujihusisha na vitendo vya rushwa kwani ni adui wa haki.
Bw. Nyakizee amesema warsha hiyo ni muendelezo wa jukumu la TAKUKURU kutoa elimu kwa umma kwa taasisi na makundi mbalimbali ili kutatua matatizo ya ukatili wa kijinsia na watoto ambalo ni jambo kubwa ndani ya jamii hasa Wilaya ya Kinondoni.
“Tumetoa elimu kwa viongozi wa Serikali za Mitaa, Jeshi la Polisi Dawati la Jinsia na Ustawi wa Jamii ili kuwezesha kutokomeza vitendo vya ukatili wa kijinsia, rushwa katika jamii” amesema Bw. Nyakizee.
Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mwananyamala Dkt. Zavery Benela ameishukuru TAKUKURU Kinondoni kwa kutoa elimu kwa wafanyakazi kuhusu maadili, ukatili wa kijinsia ambapo itawawezesha kuzingatia kanuni na shaeria za kazi katika utekelezaji wa majukumu yao.
Amesema kuwa rushwa ni adui wa haki ambayo inasababisha wateja kukosa haki ya matibabu, huku akitoa hofu jamii ataendelea kuwakumbusha na kusimamia maadili ya kazi katika sekta ya afya kuzingatia uadilifu.