Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imezindua mpango wa kutoa elimu kwa watoa huduma za kifedha juu ya matumizi ya mfumo wa kidigitali ambao utawawezesha watumiaji wa huduma hizo kuwasilisha malalamiko yao kwa urahisi. Hatua hii inalenga kuimarisha utoaji wa huduma bora na kuongeza uaminifu kwa wananchi katika sekta ya fedha.
Akizungumza leo, Desemba 10, 2024, jijini Dar es Salaam wakati wa ufunguzi wa warsha maalum kwa watoa huduma za kifedha, Kaimu Mkurugenzi wa Ustawi na Huduma Jumuishi za Fedha wa BoT, Nangi Massawe, alieleza kuwa mfumo huo umelenga kutatua changamoto zinazowakumba watumiaji wa huduma za kifedha kwa haraka na ufanisi.
“Jukumu letu ni kuhakikisha mtumiaji wa huduma za kifedha anapata haki yake. Kupitia mfumo huu, mtumiaji ataweza kuwasilisha malalamiko kwa kutumia simu yake au kompyuta, na sisi tutayashughulikia kwa haraka. Hii ni hatua muhimu ya kurejesha imani kwa huduma za kifedha na kuvutia wananchi wengi zaidi kuzitumia,” alisema Massawe.
Massawe pia alibainisha kuwa mfumo huo, ambao tayari umekamilika, unatarajiwa kuzinduliwa rasmi ifikapo Januari 2025. Alisisitiza umuhimu wa watoa huduma za kifedha kuelewa na kuutumia mfumo huo ili kuhakikisha mafanikio ya juhudi hizi za kuboresha huduma za kifedha nchini.
Kaimu Meneja wa Idara ya Ulinzi wa Watumiaji wa Fedha, Dk. Hadija Kishimba, alieleza kuwa mfumo huu utaondoa changamoto ya malalamiko kuchelewa kushughulikiwa kutokana na taratibu za zamani za kutumia matawi au dawati maalum.
“Tunataka mwananchi aweze kuwasilisha malalamiko moja kwa moja kupitia kiganja chake. Mfumo huu utasaidia kuleta ufanisi, na tunahimiza taasisi zote za kifedha kuhakikisha zinaupokea na kuutumia vizuri,” alisema Dk. Kishimba.
Elizabeth Mhina, mmoja wa washiriki wa warsha hiyo kutoka Benki ya NMB, alisema kuwa mfumo huu mpya utasaidia kupunguza wizi wa mtandaoni na kuwaelimisha wananchi kuhusu ulinzi wa taarifa zao binafsi.
“Watumiaji wengi wa huduma za kifedha hawakuwa na uelewa wa kutosha kuhusu usalama wa taarifa zao. Mfumo huu utatoa jukwaa la kuripoti changamoto kama hizi na kupata msaada wa haraka,” alieleza Mhina.
Kwa hatua hii, Benki Kuu ya Tanzania inaonyesha dhamira ya dhati ya kuboresha sekta ya fedha na kuhakikisha kuwa huduma za kifedha zinapatikana kwa usawa na ufanisi kwa wananchi wote.