Afisa Habari wa Simba SC, Ahmed Ally, ameweka wazi kuwa klabu hiyo imejipanga vyema kwa mchezo wao wa tarehe 15. Akizungumza leo, Ahmed amesema kuwa mikutano ya maandalizi sasa inafanyika katika matawi ya klabu badala ya hoteli au ofisini kama ilivyokuwa awali.
“Tuko hapa kuelezea mchezo wetu wa tarehe 15. Hapo awali mikutano kama hii tulikuwa tunafanyia ofisini au hotelini, lakini kwa sasa tunafanyia kwenye matawi yetu. Tunataka matawi ya Simba yawe na nguvu, yawe na ubora, ndiyo maana tunataka matawi ya Simba yawe na ofisi,” alisema Ahmed Ally.
Kuhusu wachezaji, Ahmed Ally alitoa taarifa za maendeleo ya afya ya baadhi ya wachezaji wa Simba SC:
Ahmed alibainisha kuwa mlinda mlango Aishi Manula alikumbwa na changamoto za kiafya siku ya safari kwenda Algeria na kwa sasa anaendelea na matibabu. “Tutawajulisha hali yake mara itakapokuwa tayari,” alisema.
Mchezaji Abdurazak Hamza aliumia katika mchezo dhidi ya CS Constantine, lakini kwa mujibu wa madaktari, hali yake si mbaya. “Anapokea matibabu na Alhamisi ataanza mazoezi,” alisema Ahmed.
Taarifa njema zimetolewa kuhusu mchezaji Yusuf Kagoma ambaye sasa amepona kabisa na yuko tayari kujiunga na timu. “Kabla ya safari ya kwenda Algeria, Kagoma alikuwa amepona, lakini mwalimu alimpa muda zaidi wa kujiandaa. Sasa ataingia kambini kujiandaa na mchezo wa Jumapili,” aliongeza Ahmed Ally.
Simba SC inatarajiwa kuonyesha kiwango bora katika mchezo huo, huku ikitegemea mchango wa wachezaji wake waliopona ili kufanikisha malengo ya klabu.