Na Mwandishi wetu, Mirerani
WAUMINI wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Usharika wa Mirerani, Jimbo la Arusha Mashariki, Dayosisi ya Kaskazini kati, Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, wametembea na kuombea amani ya nchi katika maadhimisho ya miaka 63 ya uhuru wa nchi.
Mchungaji wa KKKT, usharika wa Mirerani, Loishiye Godson Laizer, ameongoza matembezi hayo kutoka kwenye Kanisa hilo hadi katika ukuta unaozunguka migodi ya madini ya Tanzanite mji mdogo wa Mirerani.
Mchungaji Laizer, akizungumza baada ya matembezi hayo yaliyohitimishwa na maombi amesema lengo ni kuombea amani ya nchi, kuwaombea viongozi na jamii kwa ujumla ili Tanzania iendelee kuwa nchi salama.
“Tumekutana kwa ajili ya maombi mara baada ya matembezi ya amani na tunawapongeza wote waliojitokeza pia tunamshukuru Mungu kwa kusimama na sisi hadi tukamaliza jambo hili,” amesema Mchungaji Laizer.
Afisa mtendaji mkuu wa mamlaka ya mji mdogo wa Mirerani Isack Mgaya akizungumza baada ya kupokea matembezi hayo amewapongeza viongozi na waumini wote walifanikisha suala hilo.
Mgaya amesema amemwakilisha Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro mwalimu Fakii Raphael Lulandala katika kupokea matembezi hayo ya kuadhimisha sikukuu ya uhuru wa nchi.
“Watu wa imani mbalimbali tuendelee kuliombea Taifa letu na kumuombea Rais Samia Suluhu Hassan aendelee kuliongoza Taifa kwa amani na uadilifu mkubwa katika kulisimamia Taifa kiuchumi, miundombinu, kijamii, kidini na kuheshimisha matunda ya uhuru,” amesema.
“Hapa kata ya Mirerani kuna mambo mbalimbali ya maendeleo yakiyofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan ikiwemo ujenzi barabara ya lami kutoka mita 50 tuu hapa tulipo, kituo cha afya Tanzania kcha kata ya Mirerani ambapo fedha taslimu shilingi milioni 500 zimewekwa,” amesema.
Mgaya amesema miundombinu mingine na huduma za kijamii zinazidi kuimarishwa katika nyanja mbalimbali za uchumi hivyo zinazidi kuendelea vyema.
Mchungaji wa Kanisa la Anglikana Mirerani Amon Salmon Nzikobankunda amesema wameshiriki pamoja katika kuliombea Taifa na viongozi wake ili amani izidi kutawala kwa jamii.
“Baadhi ya watu wa nchi nyingine wanatamani kuwa na Taifa kama Tanzania kutokana na amani na mshikamano uliopo ila wanashindwa kwa vile wamezungukwa na vita na vurugu,” amesema.