Naibu Waziri Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Cosato Chumi (Mb.) kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Mahmood Thabit Kombo (Mb.) ameongoza Ujumbe wa Tanzania katika Majadiliano ya Ushirikiano kati ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Umoja wa Ulaya yanayofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam tarehe 10 Desemba, 2024.
Majadiliano hayo pamoja na masuala mengine yanaangazia masuala ya ushirikiano kati ya pande hizo mbili ikiwemo: Uhusiano wa uwili kati ya Tanzania na Umoja wa Ulaya na masuala ya Utawala bora, Maendeleo ya Kanda na Kimataifa na Ushirikiano katika masuala ya Usalama.
Akifungua majadiliano hayo, Mhe. Chumi amesisitiza umuhimu wa kuendelea kuimarisha ushirikiano na hatua zilizochukuliwa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kufanya mageuzi katika sekta mbalimbali hususan ushirikishwaji wa sekta binafsi, usimamizi wa masuala ya utawala bora na demokrasia, utunzaji wa mazingira na matumizi ya nishati safi na kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji.
Naye Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika mashariki, Mhe. Balozi Said Shaib Mussa katika salamu zake za ufunguzi amewapongeza wadau waliojitoa kufanikisha kufanyika kwa majadiliano hayo na amesisitiza umuhimu wa kuendeleza ushirikiano katika maeneo mbalimbali ya ushirikiano yaliyokubaliwa kati ya Tanzania na Umoja wa Ulaya kwa maendeleo endelevu.
Kwa upande wa Mwenyekiti Mwenza ambaye pia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Umoja wa Ulaya anayeshughulikia Kanda ya Afrika katika Kurugenzi ya Huduma za Nje ya Umoja wa Ulaya ( European External Action Services – EEAS) Mhe. Balozi Rita Maria Laranjinha amesisitiza dhamira ya Umoja wa Ulaya kuendelea kushirikiana na Tanzania ili kuyafikia malengo ya ushirikiano wa uwili, kikanda na kimataifa. Hatua ambayo itaziwezesha pande zote mbili kutafuta suluhu ya pamoja katika changamoto mbalimbali za kidunia ikiwemo masuala ya amani na ulinzi, afya, demokrasia na mabadiliko ya Tabianchi na kufungua maeneo mapya ya ushirikiano.
Majadiliano hayo kwa upande wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar yamehudhuriwa na Makatibu Wakuu, Wakuu wa Taasisi na Maafisa Waandamizi kutoka katika Wizara, Idara na Taasisi. Vilevile, ushiriki wa Umoja wa Ulaya umehusisha Mabalozi Wanachama wa Umoja wa Ulaya wenye makazi jijini Dar es Salaam na jijini Nairobi, Kenya.
Majadiliano hayo ni muhimu kwa Tanzania kwa kuwa yanaendeshwa kwa mujibu wa Mkataba wa Samoa, uliosainiwa mwaka 2023, ambao unachukua nafasi ya Mkataba wa Cotonou, unaoelekeza umuhimu wa kuwa na majadiliano ya mara kwa mara kati ya Umoja wa Ulaya na nchi za Afrika, Karibiani na Pasifiki (ACP). Tanzania ikiwa mwanachama wa nchi za ACP inaendelea kutekeleza wajibu wake wa kushiriki kikamilifu katika majadiliano hayo muhimu kila mwaka kwa lengo la kuimarisha ushirikiano wa kimkakati na Umoja wa Ulaya ili kukuza ubia wa maendeleo.