Na Mwandshi Wetu
UONGOZI wa Azam FC unayofuraha kuwataarifu kuwa umekamilisha usajili wa kiungo wa kimataifa wa Zimbabwe, Never Tigere, kwa mkataba wa mwaka mmoja.
Tigere aliyekuwa akichezea Platinum ya Zimbabwe, usajili wake ni pendekezo la benchi la ufundi la Azam FC, ambalo lilimfuatilia kwenye mechi kadhaa alizoichezea Platinum katika Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu.
Nyota huyo anayemudu kucheza namba sita, nane na saba, hadi anaondoka Platinum amefanikiwa kuifungia mabao manne kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika, ambayo iliingia hatua ya makundi ya michuano hiyo mwaka huu.
Mzimbabwe huyo amesaini mkataba rasmi wa kuichezea Azam FC, jana Jumatatu usiku dakika chache mara baada ya kutua nchini, zoezi lililosimamiwa na Ofisa Mtendaji Mkuu, Abdulkarim Amin ‘Popat’, huku wakala wake, George Deda akishuhudia.
Huo ni usajili wa pili kwa Azam FC kwenye dirisha dogo la usajili, wa kwanza akiwa ni kiungo mshambuliaji, Khleffin Hamdoun kutoka Mlandege.