Dkt. Hassan Abbas Katibu. Mkuu wizara ya Maliasili na Utalii akizungumza na waandishi wa habari Leo Disemba 8, 2024 jijini Dar es Salaam kuhusu uzinduzi wa tuzo za kitaifa za uhifadhi na Utalii utakaofanyik Disemba 20.2024.
Dkt. Hassan Abbas Katibu. Mkuu wizara ya Maliasili na Utalii akionesha tuzo mbalimbali za kitaifa ambazo Tanzania imejinyakulia kutokana na vivitio vyake vya Utalii na uhifadhi wakati akizungumza na waandishi wa habari Leo Disemba 8, 2024 jijini Dar es Salaam kuhusu uzinduzi wa tuzo za kimataifa za uhifadhi na Utalii utakaofanyika.
…………………
NA JOHN BUKUKU- DAR ES SALAAM
Serikali kupitia Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Hassan Abbas, imeandaa Tuzo rasmi za Kitaifa za Utalii na Uhifadhi kwa lengo la kutambua na kuenzi mchango wa sekta hiyo muhimu. Tuzo hizo, zinazotarajiwa kuzinduliwa rasmi Desemba 20, 2024, katika Hoteli ya Mount Meru jijini Arusha, ni sehemu ya juhudi za kuimarisha maendeleo ya sekta ya utalii na uhifadhi nchini.
Akizungumza na waandishi wa habari leo, Desemba 8, 2024, katika ofisi za Bodi ya Utalii jijini Dar es Salaam, Dkt. Abbas alisema kuwa uzinduzi huu ni hatua muhimu katika kutoa heshima kwa wadau wa utalii na uhifadhi ndani ya nchi. Alibainisha kuwa kwa miaka mingi, Tanzania imekuwa ikitambuliwa na kupewa tuzo za kimataifa kwa juhudi kubwa zinazofanyika katika sekta ya utalii na uhifadhi, lakini haijawahi kuwa na tuzo rasmi za kitaifa.
Dkt. Abbas alisisitiza umuhimu wa sekta ya utalii katika uchumi wa Tanzania, akisema:
“Utalii ndio sekta inayoongoza kwa kuchangia mapato ya fedha za kigeni nchini. Sekta hii inachangia zaidi ya asilimia 25 ya fedha zote za kigeni zinazoingia nchini na inatoa ajira kwa mamilioni ya Watanzania moja kwa moja na kwa njia zisizo za moja kwa moja.”
Aidha, alibainisha kuwa juhudi za Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan zimechangia pakubwa kuendeleza sekta hiyo kupitia miradi mikubwa kama filamu za Royal Tour na Amazing Tanzania, ambazo zimeendelea kuitangaza nchi kimataifa. Filamu hizi, pamoja na jitihada za serikali za kuimarisha uhifadhi, zimeongeza idadi ya watalii wanaotembelea vivutio vya Tanzania, hali ambayo imechangia ukuaji wa uchumi.
Kwa mujibu wa Dkt. Abbas, tuzo hizi mpya zitakuwa na vipengele vingi vitakavyowahusisha wadau mbalimbali wa sekta ya utalii na uhifadhi. Lengo kuu ni kuwapa heshima wale wanaoendelea kufanya kazi kubwa katika kukuza utalii, uhifadhi, na ubunifu unaochochea maendeleo endelevu ya sekta hii.
“Hatimaye, sasa wale waliofanya vizuri kwenye sekta zetu wataweza kuwa na usiku wa kupongezwa. Tuzo hizi ni mwanzo mpya wa kuthamini kazi za ndani badala ya kutegemea utambuzi kutoka nje pekee,” alisema Dkt. Abbas.
Hata hivyo, alifafanua kuwa mwaka huu tuzo hazitatolewa kwa kushindanishwa, bali uzinduzi huu ni msingi wa maandalizi kwa ajili ya mashindano rasmi yatakayofanyika mwakani, ambapo vipengele vingi zaidi vitaongezwa.
Uzinduzi wa Tuzo hizi za Kitaifa za Utalii na Uhifadhi unatarajiwa kuimarisha hadhi ya sekta ya utalii ndani ya nchi na kuongeza hamasa kwa wadau mbalimbali kuchangia zaidi katika maendeleo yake.