Madaktari bingwa 42, waliandaliwa chini ya mpango wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, wamekamilisha utoaji wa huduma za afya kwa siku sita mkoani Mara, ambapo jumla ya wagonjwa 2,442 walihudumiwa. Aidha, wagonjwa 47 walipatiwa rufaa kwa ajili ya matibabu zaidi katika hospitali za kanda.
Dk. Osmund Dyegura, Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere (maarufu kama Kwangwa), alieleza kuwa huduma hizo zilihusisha matibabu ya kibingwa kwa siku sita na zimehitimishwa kwa mafanikio makubwa mkoani humo.
Akizungumza wakati wa kuhitimisha huduma hizo, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mara, Dk. Zabron Masatu, alifafanua kuwa katika kipindi hicho, jumla ya shilingi milioni 186 zilitumika katika kutoa huduma hizo.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara, Gerald Kusaya, alitoa shukrani kwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa mpango huo wa madaktari bingwa, akisisitiza kuwa umeleta manufaa makubwa kwa wakazi wa mkoa huo, hususan katika kupunguza changamoto za magonjwa yanayohitaji matibabu ya kibingwa. Kusaya pia aliwahimiza madaktari kuendelea kuwa na moyo wa kusaidia wananchi.
Kwa upande wake, Dk. Baraka Malegesi, mmoja wa madaktari bingwa walioshiriki, alimshukuru Rais Samia kwa mpango huo wa kusaidia Watanzania. Alibainisha kuwa bado kuna uhitaji mkubwa wa huduma za afya za kibingwa, hasa katika maeneo ya vijijini.
Mpango huu wa utoaji huduma za afya unadhihirisha dhamira ya serikali ya kuhakikisha wananchi wanapata matibabu bora na kupunguza changamoto za kiafya nchini.