Na Prisca Libaga Arusha
JUMLA ya wagonjwa 4000 wanatarajiwa kupatiwa matibabu ya kibingwa kutoka kwa madaktari bingwa na bingwa wabobezi wa magonjwa mbalimbali kwenye Hospitali ya rufaa ya Mount Meru Mkoa wa Arusha.
Mgaga mfawidhi wa Hospitali ya rufaa ya Mkoa wa Arusha Mt. Meru, Dokta Alex Ernest ameyasema hayo leo Desemba 6 alipokuwa akizindua Kambi maalumu ya madaktari bingwa na bingwa wabobezi iliyoandaliwa na Hospitali hiyo.
Amesema katika kuadhimisha miaka 63 ya Uhuru wa Tanzania bara, Hospitali hiyo imeandaa Kambi maalumu ya matibabu ambayo inaanza leo Desemba 6 hadi 9 kwa ajili ya kuwahudumia Wananchi wa Mkoa wa Arusha wenye changamoto ya afya na wanahitaji msaada wa madaktari bingwa.
Dokta. Ernest amesema lengo la Kambi hiyo ni kutaka wananchi kujionea namna ambavyo Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassani, imewekeza kwa kiwango kikubwa katika Sekta ya afya ambapo imefanya Mapinduzi makubwa.
Lengo lingine ni kuwafikia wananchi wangi wasio kuwa na uwezo wa kuwafikia madaktari bingwa na bingwa wabobezi ili wapate huduma ya matibabu kulingana na magonjwa waliyonayo.
Dkt. Alex anaeleza kuwa kambi hiyo itakuwa na madaktari bingwa na bingwa wabobezi 30 kutoka Hospitali ya rufaa ya Rufaa ya Mkoa wa Arusha Mount Meru ambapo kila siku wagonjwa 1000 watapatiwa huduma bure za matibabu pamoja na dawa.
Aidha ameongeza kuwa Magonjwa yasiyoambukuza ni moja ya changamoto kubwa kwa Wananchi hivyo watatoa Elimu itakayowasaidia wananchi kubadili mtindo wa maisha ili kuepukana na magonjwa hayo.