Na Ashrack Miraji Fullshangwe Media
Tanga – Mkuu wa Wilaya ya Korogwe, Mhe. Mwakilima, amefunga rasmi Mkutano wa Mwaka wa Wanajiosayansi 2024 uliofanyika jijini Tanga. Mkutano huo ulijumuisha wataalamu wa masuala kutoka ndani na nje ya nchi,
Akizungumza kwa niaba ya Mgeni Rasmi, Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Mhe. Barozi Batilda Burian, Mhe. Mwakilima alieleza furaha yake kwa kushiriki katika tukio hilo la kihistoria, akisema kuwa ni heshima kubwa kwa mkoa wa Tanga kuwa mwenyeji wa mkutano wa kimataifa wa wanajiosayansi.
“Kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Tanga na kwa heshima mliyoniipa, najivunia kuwa sehemu ya historia ya mkutano huu wa wanajiosayansi. Miongoni mwa masuala ambayo ofisi ya Mkoa imewezeshwa kufanyika ni kuhakikisha kwamba mkoa wetu unakuwa na amani na utulivu, na tunajivunia kuwa Tanga ni mkoa tulivu,” alisema Mhe. Mwakilima.
Aliongeza kuwa mkoa wa Tanga umeendelea kuimarisha ulinzi na usalama, na kwamba ni mikutano kama hii ya kimataifa ambayo inasaidia kukuza picha ya Tanga kama kanda ya kibiashara na kisayansi.
Mkutano huu, uliojadili masuala ya madini, umekuwa wa kipekee kwa kushirikisha wanajiosayansi kutoka maeneo mbalimbali duniani. Wajiosayansi walijadili mada mbalimbali, ikiwemo mchango wa madini katika mabadiliko ya nishati chafuzi kwenda kwenye nishati endelevu na safi kwa mazingira.
Mhe. Mwakilima aliendelea kusema, “Ni matumaini yangu kuwa mada na mawasilisho haya yatatoa matokeo ambayo yatasaidia kuongeza tija katika uchumi wa taifa letu. Wanajiosayansi wataendelea kutumia maarifa yao katika kuboresha sekta ya madini na nishati.”
Aidha, Mhe. Mwakilima aliongezea kuwa mkoa wa Tanga umebarikiwa kwa kuwa na rasilimali nyingi za madini, na alitoa wito kwa wanajiosayansi kuendelea kufika Tanga kufanya tafiti mbalimbali za kisayansi.
“Tunaendelea na tafiti kuhusu mafuta na gesi asilia, na tunataka kuona wataalamu wa kisayansi wakifanya tafiti zaidi. Hizi tafiti zitasaidia kuleta maendeleo ya kiuchumi kwa mkoa wetu na taifa kwa ujumla,” alisisitiza.
Katika hotuba yake, Mhe. Mwakilima alisisitiza umuhimu wa wanajiosayansi kuzingatia maadili ya kitaaluma, hasa kuhusiana na usajili wa wataalamu wa sayansi nchini. Alitoa rai kwa Rais wa Jumuhiya ya Wanajiosayansi Tanzania, Dkt. Risante Mshiu, kuhakikisha kwamba wataalamu wote wamesajiliwa ili kuepuka matumizi ya njia zisizo za kitaaluma ambazo zinaweza kuathiri tasnia ya sayansi.
“Serikali lazima ione umuhimu wa kutoa kipaumbele kwa tahaluma hii. Nitasimamia changamoto hii na kuiwasilisha kwa Mkuu wa Mkoa ili tuweze kuona namna bora ya kusimamia wataalamu wa sayansi,” alimalizia kusema Mhe. Mwakilima.