Waziri wa Katiba na Sheria, Profesa Palamagamba Kabudi, akifungua kikao kazi kati ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Wanasheria pamoja na Mawakili wa Serikali kutoka idara na vitengo mbalimbali, leo, Desemba 6, 2024, jijini Dodoma.
Mwanasheria Mkuu wa Serikali Bw. Hamza Johari akizungumza katika kikao kazi kati ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Wanasheria pamoja na Mawakili wa Serikali kutoka idara na vitengo mbalimbali, leo, Desemba 6, 2024, jijini Dodoma.
Katibu Mkuu Wizara ya Sheria na Katiba Eliachim Maswi akizungumza katika kikao kazi hicho.
……………..
NA JOHN BUKUKU, DODOMA
Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Hamza Johari, amewataka Wanasheria na Mawakili wa Serikali kuwa huru katika kuchangia mada mbalimbali, kutoa maoni na mapendekezo ya kuboresha huduma za kisheria serikalini pamoja na kutafuta njia bora za kukabiliana na changamoto zinazokabili sekta ya sheria nchini.
Akizungumza leo, Desemba 6, 2024, jijini Dodoma katika kikao kazi kati ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Wanasheria pamoja na Mawakili wa Serikali kutoka idara na vitengo mbalimbali, Johari amesema kikao hicho kinalenga kujadili utekelezaji wa miongozo ya ofisi yake na kubaini vikwazo vinavyokwamisha utendaji wa mawakili wa serikali.
“Kupitia kikao hiki, tutajadili namna bora ya kuandika mikataba ili kupunguza changamoto zinazojitokeza wakati wa utekelezaji, hasa katika kesi za kimataifa, kuhakikisha serikali inashinda na kuepuka gharama kubwa za fidia,” alisema Johari.
Aidha, ameongeza kuwa ofisi yake itatoa mrejesho kwa wakurugenzi na wakuu wa vitengo vya sheria serikalini kuhusu utekelezaji wa maazimio ya vikao vilivyopita. Pia wataendelea kukusanya maoni na mapendekezo ya kukabiliana na changamoto za sekta ya sheria kwa lengo la kuweka mikakati ya pamoja ya kutatua matatizo yaliyopo.
Kwa upande wake, Waziri wa Katiba na Sheria, Profesa Palamagamba Kabudi, amewataka wanasheria na mawakili wa serikali kutumia fursa ya kikao hicho kujadiliana kwa kina namna ya kuboresha huduma za kisheria serikalini, hasa katika kutoa ushauri na muongozo wa kisheria unaozingatia Katiba na sheria za nchi.
“Moja ya changamoto kubwa ni usimamizi wa mikataba baada ya kusainiwa. Kikao hiki ni muhimu kwa sababu kinatoa fursa ya kuboresha huduma za kisheria na kuhakikisha nchi inabaki na amani na ustawi kwa wananchi wake,” alisema Profesa Kabudi.
Amesema wizara yake imefanya mabadiliko kadhaa, ikiwa ni pamoja na kuongeza watumishi kwa ajili ya kuimarisha usimamizi wa sheria, hususan sheria za mwaka 2017 zinazohusiana na mali asilia na rasilimali za nchi.
Profesa Kabudi pia alieleza kuwa mabadiliko ya kiuchumi na teknolojia duniani yanalazimisha mataifa kuboresha sheria zao ili kuendana na mahitaji ya wakati na kuhakikisha wananchi wanapata maendeleo endelevu.
“Natarajia kikao hiki kitazalisha mapendekezo muhimu ya kuboresha maeneo ya kisheria ili nchi yetu iwe kitovu cha uwekezaji na maendeleo kwa wananchi wote, kama ilivyoelezwa kwenye Ibara ya 9 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,” alisema.
Aidha, amesisitiza umuhimu wa kuimarisha mafunzo kwa wanasheria, akieleza kuwa kazi ya wanasheria wa serikali haipaswi kuhusishwa tu na kuendesha kesi.
“Tunaangalia uwezekano wa kuanzisha chuo cha kuwanoa mawakili wa serikali ili kuwapa ujuzi mpana zaidi na kuwatoa kwenye dhana potofu kwamba kazi yao ni kusimamia mashauri na mashtaka pekee,” aliongeza Profesa Kabudi.