Na SOPHIA KINGIMALI.
CHUO cha Ufundi Stadi cha Furahika (VETA)kimeanzisha program mpya ya kuwafundisha watoto wa kike masuala ya ukondakta kwenye mabasi ili kuifanya kazi hiyo kwa maadili na maslahi kwa Taifa na kwa jamii yao.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Mkuu wa Chuo hicho, Dkt. David Msuya amesema kozi hiyo inatolewa bure na wanapokea wasichana kutoka Mikoa mbalimbali.
Amesema kozi hiyo itafundishwa kwa muda wa siku zisizozidi 10 na kisha mwanafunzi atapewa cheti cha Veta.
“Nichukue fursa hii kuwaita wasichana kutoka Mkoa wa Tanga, Iringa, Songea, Mbeya, Mwanza, Shinyanga, Kahama, Geita, Mara, Musoma, Lindi, Mtwara, Dar es Salaam, Manyara na Arusha kuja Chuo cha Furahika kujifunza masuala ya ukondakta kwenye mabasi.
“Fani hii mwanafunzi anasoma siku 10 tu, kisha tutampatia cheti cha Veta…ni bure kabisa. Hivyo tunawakaribisha watu wote wanaotaka kujifunza, lengo ni kuunga mkono juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt Samia Suluhu Hassan ili watu waweze kujiajiri na kuajiriwa,” amesema na kuongeza kuwa:
“Kozi hii ni mpya, kwa wasichana wote, warembo wasikae nyumbani waje wasome na uzuri wa kozi hii hata wa darasa la saba anasoma kwasababu anachojifunza ni customer care kwa mteja na vile vitu ambavyo vinamuhitaji ndani ya gari,”.
Amesema kuwa dirisha la usajili limefunguliwa hivyo wanaweza kujiunga kupitia mfumo au kufika chuoni hapo.
Ameongeza kuwa, wanaamini katika kujifunza masomo mbalimbali ya Veta ni njia pekee ya kufanya kijana aondokane na mawazo mabaya.
“Kwahiyo tunaomba wazazi wasiwaache watoto, wawalete waje kujifunza kozi mbalimbali tunazotoa. Lakini kimsingi tunaamini Tanzania ya mama Samia tunahitaji vijana wenye ujuzi ili kwenda na kasi ya soko la ajira.
“Kusoma tu chuo haitoshi, kuna watu Wana degree, PhD lakini anatembea tu na vyeti bila kuwa ujuzi haisaidii. Vyuo vinafundisha kama biashara havifundishi kuwasaidia ujuzi wa maisha…tunaamini kwamba Tanzania kuna nafasi za ajira kwa kampuni nyingi binafsi lakini watu wanasoma kozi ambazo hazina ajira,” amesema.
Amefafanua kuwa, fursa zipo nyingi isipokuwa watu wengi wanashindwa kutumia fursa na kuilaumu serikali.
“Serikali haiwezi kukuletea vitu nyumbani, kuna vitu lazima sisi wenyewe tupambane kuhakikisha Tanzania ya mama Samia inawezekana kupitia Kampuni zetu na ajira zinapatikana.
“Na ajira zipo Wafanyabiashara wanatoa ajira, kampuni binafsi zinatoa ajira. Hivyo waje Furahika kusoma kozi mbalimbali tunazotoa bure kabisa,” amesisisitiza.