Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe, Dkt. Ali Mohamed Shein, akiwatunuku vyeti wanafunzi waliofanya vizuri katika masomo yao katika Mahafali ya 23 ya Chuo Kikuu Mzumbe yaliyofanyika leo Disemba 5, 2024 katika Kituo Cha Mikutano cha Julius Nyerere jijini Dar es Salaam
Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe, Dkt. Ali Mohamed Shein, akizungumza jambo katika wakati Mahafali ya 23 ya Chuo Kikuu Mzumbe yaliyofanyika leo Disemba 5, 2024 katika Kituo Cha Mikutano cha Julius Nyerere jijini Dar es Salaam.
………….
NA NOEL RUKANUGA, DAR ES SALAAM
Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe na Rais Mstaafu wa Zanzibar Dkt. Ali Mohamed Shein amewataka wahitimu wa chuo hicho kufanya kazi kwa bidii ili kujiletea maendelea, huku akiwakumbusha kutumia maarifa waliyopata chuo kutengeneza fursa za ajira na sio kusubiri kujajiriwa.
Akizungumza leo Disemba 5, 2024 jijini Dar es Salaam Mahafali ya 23 ya Chuo Kikuu Mzumbe, Kampasi ya Dar es Salaam, yaliyofanyika katika Kituo Cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC) Dkt. Ali Mohamed Shein, amesema kuwa mafanikio ya elimu waliyopata yana nafasi kubwa ya kufanikiwa kimaisha hata katika mifumo isiyo rasmi ya ajira.
Dkt. Shein amesema kusoma ni njia moja katika kutafuta maisha, na kwamba hakuna njia ya mkato katika mchakato huo, huku akiwapongeza kwa mafanikio waliyoyapata katika hatua hiyo kielimu na kuwatakia kila la kheiri wanapoingia katika hatua ya tatu ya ushindani kwenye soko la ajira.
Amesema kuwa kusoma ni miongoni mwa njia katika kutafuta maisha na katika hilo hakuna njia ya mkato, huku akisisiiza kuwa Elimu haina mwisho hivyo wanapopata nafasi wanaweza kujiendeleza na kufika mbali.
“Jitihada kubwa mmeonesha kuwa mnaweza kujipambania na hiyo ni uthibitisho kwamba mnaweza manweza kujipambania katika soko la ushindani wa ajira, wito wangu kwenu ni kwamba msichague kazi, msisubiri kuajiriwa serikalini, tumieni elimu kujiajiri.
Amesema kuwa kuhitimu chuo ni mwanzo wa mitihani ya maisha, hivyo amewataka kujiandaa pamoja na kuwa na hamu kubwa ya kutaka kusonga mbele katika mafanikio.
“Soko la ajira lina ushindani mkubwa, mjitahidi kutafuta ajira, ila kumbukeni hili mlilosikia kuwa mtu aliyehitimu chuo 1995, hakupata ajira, lakini akachagua kujiajiri Sekta ya Ufugaji, akachagua afuge kuku, kuliko kukaa bure kusubiri ajira ya serikalini na kimsingi ufugaji wa kuku una tija kubwa.
Mwenyekiti wa Baraza la Chuo Kikuu Mzumbe, Profesa Saida Yahya-Othman, amewapongeza wafanyakazi wa chuo kwa kazi kubwa na adhimu wanayoendelea kuifanya ya kuwaandaa vijana, na kwamba anaamini wanaohitimu hao wako tayari kuikabili dunia na changamoto zake.
Profesa Saida amesema “Niwapongeze wahitimu wote mtakaotunukiwa Stashahada, Astashahada na Shahada leo, juhudi na uvumilivu mliouonesha kipindi chote cha masomo yenu, hakika zinawastahilisha vyeti mnavyopokea leo.
“Tunaposherehekea mafanikio ya kuhitimu masomo yetu, tufanye tafakuri ya maisha yetu ya chuoni na yale ya baadaye, na changamoto zitazotukabili katika soko la ajira, na katika maisha yetu kwa ujumla, Changamoto ni nyingi, na zimeathiri kwa kiasi kikubwa mfumo wa kiutendaji na ajira” amesema Profesa Saida.
Amesema kuwa “Tukumbuke huu ndiyo mwanzo wa elimu yetu ya ulimwengu. Wale waliowahi kupata barua pepe kutoka kwangu, watakuwa wameiona nukuu ya Mwalimu Nyerere mwisho wa kila ujumbe wangu isemayo: “A man stops himself from thinking if he assumes that anyone exists who cannot teach him something.”
Profesa Saida amesema kuwa kutunukiwa kwao shahada, hata kama ya uzamivu, isiwafanye kufikiri kuwa wanajua yote, “Hata kuwa tunajua mengi, kwani kwenye dunia ya leo, kila tujuacho ni tone baharini. Na ulimwengu una mengi ya kutufundisha nje ya darasa. Tusimdharau yeyote kuwa hajui”
Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe Profesa William Mwegoha, amesisitiza umuhimu wa kutochagua kazi badala yake kuwekeza nguvu katika kujiajiri kwani ni njia rafiki ya kufikia malengo.
Amewataka wahitimu kupambana bila kuchoka pamoja na kujenga matumaini na ujasiri pamoja na kuepuka kukata tamaa katika maisha.