Na Sophia Kingimali.
Waziri wa fedha Dkt. Mwigulu Nchemba amesema mpango wa kunusuru kaya maskini wa awamu ya tatu utakuwa mpango jumuishi na utaendana na dira ya maendeleo ya Taifa inayoandaliwa ya 2025-2050.
Hayo ameyasema leo jijini Dar es salaam katika majadiliano ya ngazi ya juu kati ya serikali na wadau wa maendeleo kuhusu mustakabali wa awamu ya tatu ya mpango wa kunusutu kaya maskini chini ya mfuko wa maendeleo ya jamii nchini(TASAF).
Amesema mpango huo utakuwa jumuishi na hautoacha mtu nyuma kwani utahakikisha unawezesha wananchi wa hali ya chini kushiriki katika miradi ya maendeleo inayoendelea nchini.
“Uundaji wa mpango huu wa tatu wa TASAF utahusisha shughuli za uzalishaji ambazo hazitabangua sehemu ya jamii yetu kwani makundi yote katika jamii yatahusishwa katika shughuli za maendeleo na mgawanyo wa bajeti kwa ajili ya maendeleo hayo”,Amesema
Ameongeza kuwa Awamu ya tatu ya mpango huo inaandaliwa baada ya mafanikio makubwa yaliyopatikani katika mpango wa kwanza na wa pili kwani kumekuwa na shuhuda mbalimbali kutoka kwa wanufaika wa mpango huo ambao vipato vyao vimeongezeka kutoa hatua moja kwenda nyingine.
Kwa upande wake Mwakilishi mkaazi wa benki ya Dunia Nathan Belete amesema benki ya Dunia imeahidi kutoa kiasi cha takribani Dola za marekani milioni 300 ili kusaidia awamu hii ya tatu ya kunusuru kaya maskini.
Amesema wameamua kutoa fedha hizo kwani mpango huo wa tatu ni mfano wa kuigwa Duniani kwani umesaidia kukabiliana na umaskini na kuonyesha matokeo chanya.
Naye Waziri wa Waziri wa nchi ofisi ya waziri mkuu (kazi,vijana,ajira na watu wenye ulemavu) Ridhiwan Kikwete amesema ili kuendeleza kwa mafanikio makubwa mradi huu wa awamu ya tatu serikali imejipanga kushirikiana na wadau wa maendeleo kuhakikisha mpango huu unafanikiwa kwa kiasi kikubwa na kuleta matokeo chanya kwa Taifa na wananchi ambao ndio walegwa wakuu.
Akizungumzia kwa upande wa Zanzibar Waziri wa nchi ofisi ya Rais fedha na uchumi Dkt Saada Mkuya amesema mradi wa TASAF umeseidia katika maeneo mengi ikiwemo ujenzi wa skuli,hospital lakini pia kuwafikia baadhi ya familia na kuwaanzishia miradi mbalimbali ikiwemo ufugaji wa kuku.